Monday 22 August 2016

VIGOGO NYANZA MAJI SHINGONI


WAKATI serikali ikifanya uchunguzi na kuwahoji baadhi ya waliokuwa vigogo wa Chama Kikuu Cha Ushirika Mkoa wa Mwanza cha Nyanza (NCU 1964 Ltd), baadhi ya vigogo hao wanadaiwa kukutana na kufanya vikao vya siri na wale walionunua mali za NCU kwa bei chee.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka kwa watu wa karibu na vigogo hao, zimedai kuwa baadhi ya wanunuzi na viongozi hao wa zamani wa Nyanza, wamekutana mara mbili wiki iliyopita, katika maeneo tofauti jijini hapa.

Kukutana kwa vigogo na wanunuzi walioitafuna Nyanza, kumekuja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuagiza waliofuja mali za NCU kushughulikiwa, ikiwa pamoja na kuzirudisha zilikouzwa.

Kwa mujibu wa habari hizo, kikao cha kwanza kilichowakutanisha wahusika wachache, kilifanyika mtaa wa Uhuru, wilayani Nyamagana, kwenye hoteli maarufu (jina tunalo).

Kikao cha pili, ambacho kilihusisha wahusika wengi, akiwemo mwakilishi wa kampuni moja kutoka jijini Dar es salaam, inayomiliki moja ya viwanda vya NCU, kilichonunuliwa hapa, kilifanyika maeneo ya Nyegezi, wilayani humo.

“Kikao chao cha kwanza hakikuwa cha mafanikio zaidi, kilihusisha watu wachache, wakaazimia kukutana tena mara ya pili ili kuweka mikakati ya kukabiliana na rungu la serikali, ambalo limeanza kuwasaka baadhi yao ili kuhojiwa,” kilidokeza chanzo hicho.

Kiliongeza: “Kikao cha Nyegezi kilihudhuriwa na wahusika wengi, akiwemo mwakilishi wa kampuni moja kutoka jijini Dar es Salaam, ambayo inamiliki kiwanda kimoja. Waliweka mikakati mbalimbali ya kujinasua, ikiwemo kuteua baadhi ya watu wa kwenda kumuona Rais."

Mbali na mwakilishi wa kampuni hiyo, wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na aliyekuwa meneja wa zamani, mwenyekiti, mjumbe wa bodi, wahasibu wawili na mnunuzi wa kiwanda kimoja cha kuchambua pamba.

Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa polisi mkoani Mwanza, ambaye hakutaka kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, wiki iliyopita, alikiri kuanza kuhojiwa kwa baadhi ya vigogo wa zamani wa Nyanza kuhusiana na sakata hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo, bila kufafanua, alisema mwishoni mwa wiki kuwa, vyombo vya habari vitataarifiwa leo (Jumatatu), hatua ambazo kamati yake inachukua.

Akitoa maagizo ya kushughulikia mali za Nyanza, kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, Agosti 11, mwaka huu, Rais Magufuli alisema:

"Polisi na mkuu wa mkoa mko hapa,  haiwezekani mali za wanyonge zikawa zinachezewa, lazima zirudi, ushirika wa Nyanza ulikuwa na Ginnery nyingi, lakini sasa zimekufa.”

Rais Magufuli alisema aliyenunua kiwanda cha New Era kwa bei chee ya sh. milioni 30, badala ya zaidi ya sh. bilioni moja, sasa hakitumii kama kiwanda cha mafuta na kwamba, kilimo cha pamba kimeshuka, na kinaelekea kufa kwa sababu ya kuua Nyanza, kwa kutafuna mali zake kwa maslahi ya matumbo ya watu binafsi, hali inayosababisha wakulima wa zao hilo kuteseka na kukata tamaa.

“Mkuu wa mkoa, tunalipwa mishahara, tujipange kwa majukumu ya wananchi hawa, tusipofanya hivyo tutahukumiwa siku moja, kama siyo hapa basi mbinguni. Mali za Nyanza zirudi mikononi mwa wenyewe,” alisisitiza Rais Magufuli.

Alizitaja Ginnery zingine za ushirika huo, zinazomsikitisha kutokana na kufa kwake ni pamoja na Manawa, Kasamwa, Buchosa, Buyagu na Nassa.

No comments:

Post a Comment