Monday 22 August 2016

PROFESA LIPUMBA AIPASUA CUF, WAJUMBE WARUSHIANA VITI UKUMBINI


HALI si shwari ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), baada ya makundi ya wanachama wanaopingana, kurushiana viti wakati wa mkutano mkuu maalumu.

Tukio hilo lilitokea jana, wakati wa mkutano huo, ulipofanyika kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Awali, makundi ya wanachama yanayopingana, yalitaka kushikanamashati wakati wa mkutano huo, kila moja likililaumu kundi lingine kuhusu mvutano ulioibuka ndani ya chama hicho.

Baada ya mvutano huo na kutoleana maneno makali, hatimaye makundi hayo mawili ya wanachama, yalianza kurushiana viti, hali iliyotishia usalama ukumbini.

Mvutano huo uliibuka baada ya kundi linalodaiwa kumuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kupinga kile walichodai kuingiliwa kwa masuala ya ndani ya chama hicho kunakofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Malalamiko hayo yalisababisha kuibuka kwa kundi lingine linalodai kumpinga Lipumba, hivyo kutaka wanachama wanaomuunga mkono waondoke kwenye mkutano huo.

Wakati msuguano huo ukiendelea, ghafla wakati Profesa Lipumba alipofika eneo la mkutano huo, wanachama wanaomuunga mkono walimfuata na kumpokea kwa shangwe huku wakimshinikiza kuendelea na nafasi yake ya uongozi.

Aidha wakati ilipowasilishwa barua ya Lipumba ya kutaka kurudi ndani ya chama hicho, kisha Kamati Kuu ya CUF kupaswa kuijadili, mvutano mkubwa uliibuka kutokana na baadhi ya wajumbe na wanachama kueleza kuwa, barua hiyo haiwezi kujadiliwa bila Lipumba kuwepo.

Katika mkutano huo ulioitishwa kwa ajili ya uchaguzi wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, mizengwe ilianza kuonekana kwa viongozi wa CUF, ambao hawamtaki Lipumba, kuanza kutengeneza mazingira ya kutojadiliwa kwa barua ya Lipumba ya kutaka kurejea kwenye nafasi yake.

Mapema, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, aliwaeleza waandishi wa habari kuhusu ajenda za mkutano huo, lakini suala la Lipumba aliliweka kapuni kulizungumzia.

Baada ya kubanwa na waandishi wa habari, Mketo alilazimika kulizungumzia suala hilo kwa kusema kuwa barua yake itajadiliwa.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa CUF walisikika wakisema kuwa, barua ya Lipumba aliyoandika mwaka jana ya kujiuzulu nafasi ya uenyekitim bado haijajibiwa.

Walisema kimya hicho kilikuwa kinamaanisha kuwa, CUF inamtambua  Profesa Lipumba kama mwenyekiti.

Mzozo huo ulisababisha baadhi ya wajumbe wa mkutano huo, kushinikiza kuitwa kwa Profesa Lipumba ili ahojiwe kuhusu sababu zilizomfanya kujiengua kwenye nafasi yake.

Baadhi ya wajumbe wanaodaiwa kumuunga mkono Lipumba, walimfuta kisha kuingia naye ukumbini saa 8.45 mchana, ndipo vurugu zilipozidi kutawala na kusababisha viongozi wa chama hicho kulazimika kuomba msaada wa jeshi la polisi.

Profesa Lipumba aliingia ukumbini kwa majadaliano, ambapo saa tisa alasiri, mkutano huo uliahirishwa.

Baadaye ililazimika kura za maoni zipigwe ili kufahamu idadi ya wajumbe wanaomtaka Lipumba kuendelea na nafasi ya uenyekiti na wale wanaompinga.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya ndani vya chama hicho, baadhi ya vigogo wa CUF, walishinikiza kura hizo zipigwe kwa kuinua vidole badala ya kupigwa kwa siri.

Hatua hiyo ilikuwa mkakati wa kuwazuia wajumbe kutoa maoni yao kwa uhuru zaidi ili kutimiza azma ya kumzuia Lipumba kurejea kwenye chama hicho.

Baada ya vidole kuinuliwa, wajumbe 14 walimtaka Lipumba aendelee na nafasi hiyo huku 476, wakipinga, kati ya wajumbe halali wwa mkutano huo 832.

Kiongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho, alibainisha wazi ubakwaji wa demkorasia ya wajumbe hao, uliofanywa na viongozi wenzake kwa kuhesabu vidole kwa mtindo wa haraka haraka pasipo kuhakiki wajumbe.

“Huu ni mkakati unaoendeshwa na CHADEMA kukihujumu chama chetu. Kura zimehesabiwa haraka haraka kama ilivyokuwa kwa CHADEMA wakati wakimuidhinisha Lowassa kuwa mgombea urais, wajumbe hawakupewa fursa ya kupiga kura kwa siri kama ambavyo demokrasia inavyotaka ili kuwapa uhuru zaidi wa kufanya maamuzi,” alisisitiza kiongozi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.

Kabla ya vurumai hiyo, Mketo, alisema wanachama tisa walichukua fomu ya kugombea uenyekiti, ambapo sita walikatwa na watatu walibaki. Waliobaki ni Twaha Tasilima, Joseph Magori na Riziki Shahari Mngwali.

Alisema kwa upande wa nafasi ya Kaimu Mwenyekiti, waliochukuwa fomu ni wanne, ambapo wawili waliandika barua ya kijiengua huku wakibaki wawili katika kinyang'anyiro hicho.

"Waliojitoa ni Juma Amier Muchi na Juma Duni Haji, ambapo Juma Duni, alijitoa kwa mujibu wa katiba ya chama inavyomtaka kuwa mwanachama yeyote akijitoa kwenye chama na kwenda chama kingine, akirudi tena anapaswa kukaa miaka miwili ndipo agombee uongozi,"alisema.

Mkutano huo ulishindwa kufikia maamuzi baada ya kuvunjika saa 2.00 usiku.

No comments:

Post a Comment