Monday 22 August 2016

UVCCM YATAKIWA KUCHAGUA VIONGOZI IMARA 2017


 


JUMUIA ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Bukoba, wametakiwa kutumia uchaguzi wa ndani ya Chama utakaofanyika mwaka 2017, kuwa sehemu ya maandalizi ya kujipanga na kupata wagombea, ambao watakivusha Chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya UVCCM, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro, alisema kuwa uchaguzi huo utakuwa nafasi nzuri kwa jumuia hiyo kujipanga na kufahamu nani ashike nafasi gani.

Alisema ili Chama kipate ushindi, pamoja na mipango mingine, mgombea mwenye sifa ni mtu muhimu.

“Kuna tatizo kwenye chama la kuwa na baadhi ya watu wasio na uwezo wa kujenga hoja. Yapo mengi yanafanywa na serikali, mfano kujenga barabara, zahanati kila kijiji, shule za kata, maabara na sasa madawati, lakini haya yote yanataka yapate watu wa kuyatetea na kuwaeleza wananchi, ili waache kudanganywa eti serikali haijafanya lolote” alisema.

Kinawiro alisema lazima  wachaguliwe watu wenye uwezo wa kujenga hoja, badala ya kuchaguliwa mtu anayepanda jukwaani hadi anashuka, hajajenga hoja yoyote ya msingi na kuwataka vijana kufundishana namna ya kujenga hoja kwa manufaa ya Chama na taifa kwa ujumla.

“Lakini vijana pia mjenge utamaduni wa kusoma taarifa mbalimbali za serikali za utekelezaji wa Ilani ya CCM ili mnapokuwa majukwaani, muwe na ufahamu wa mambo gani yametekelezwa na serikali na yapi yamepangwa kutekelezwa katika maeneo yenu,” alisisitiza.

Alisema vijana ndilo jeshi la CCM katika nyanja zote za kijamii na za kiuchumi, lakini kuna viashiria vinavyoonyesha kama vile baadhi yao wamekata tamaa, badala ya kutembea kifua mbele, kwa uhakika na kujiamini, huku wakiweka uzalendo wa Chama na nchi mbele.

“Lazima vijana mpiganie chama maana hakuna jeshi jingine ndani ya CCM, jikague na ondoa unyonge, maana inawezekana wapo ambao hawajafahamu kama sasa wako katika mfumo wa vyama vingi. Katika siasa za vyama vingi, vijana lazima muweke uzalendo mbele zaidi wa nchi na chama, msipofanya hivyo mtakuwa mnakwamisha jitihada za chama,” alisema.

Aidha alisema kwa sasa inaonekana dhana ya vijana kujitolea kwa ajili ya Chama inapungua na kwamba wanahitaji kujituma zaidi na kujitoa. Alisema malipo yao ni kuitwa Chama tawala, huku akiwasisitiza kuacha makundi ndani ya Chama, ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kukibomoa badala ya kukijenga.

“Tumieni matokeo ya jimbo la Bukoba Mjini, ambalo CCM ilipoteza, lakini pia tumieni hata takwimu za ushindi Bukoba Vijijini, fanyeni tathmini ili mjue mlikosea wapi, mlianguka wapi na msimame vipi, mtaona kwamba mnapaswa kupambana kwa kiwango gani,” alisema.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Bukoba, Ashraph Kazinja, alisema waliamua kuandaa semina hiyo ili kukumbushana majukumu yao kama jumuia na pia kuweka mipango itakayosaidia shughuli za CCM kusonga mbele na kukiwezesha kuendelea kupata ushindi.

Kazinja alisema baada kuchaguliwa kushika wadhifa alionao, alifanya ziara katika kila kata na kugundua kuna udhaifu, ambao kama vijana inabidi waufanyie kazi, ikiwemo wa maadili ya uongozi na kwamba ana imani baada ya mafunzo hayo, kila kijana atatambua jukumu lake huku akionya kuwa, ambaye ataona hawezi kuendana na kasi ya sasa, ajiengue mapema.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, vijana walioshiriki katika semina hiyo ni 152. Alisema UVCCM wilaya ya Bukoba inao wanachama zaidi ya 3,000.
 

No comments:

Post a Comment