Tuesday 23 August 2016

UVCCM KUANDAMANA NCHI NZIMA AGOSTI 31


UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema wakati CHADEMA ikipanga kuitisha maandamano yasiyo na ukomo Septemba Mosi, mwaka huu, wao watatangulia kufanya hivyo Agosti  31, mwaka huu, kwa lengo la kumpongeza Rais Dk. John Magufuli.

Umesema pongezi hizo zinatokana na kuguswa na kazi nzuri inayofanywa na Dk. Magufuli na serikali yake katika kuwatumikia wananchi, ikiwa ni miezi michache tangu aingie madarakani.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alieleza hayo jana, katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Makao Makuu ya UVCCM, jijijini Dar es Salaam.

Shaka alisema mkakati wa serikali ya awamu ya tano katika uboreshaji wa huduma za jamii, ukusanyaji kodi na mapato, kukaribia kumaliza tatizo la upungufu wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari na hatua inazozichukua za kusimamia uwazi, uadilifu na uwajibikaji ni mambo yanayohitaji kuungwa mkono.

Aidha, alisema katika kipindi kifupi cha miezi tisa, tangu Rais Dk. Magufuli achaguliwe kidemokrasia Oktoba 25, mwaka jana, wananchi wameshuhudia mabadiliko makubwa serikalini, ambapo uwajibikaji, utoaji huduma, utii, nidhamu na utendaji bora umeongezeka.

"Serikali yake ina dhamira ya wazi, imekusudia kupambana na ufisadi, wizi na ufujaji mali za umma, ukwepaji kodi bandarini na kwenye viwanja vya ndege huku mara zote rais akiweka mkazo na kuwataka watendaji na wataalamu wa serikali kutokaa ofisini, bali wawaendee wananchi na kuwatatulia kero,"alisema.

Alisema Dk. Magufuli amekuwa akiwahimiza viongozi na wataalamu kufuatilia matatizo, kutatua kero na shida za wananachi, iwe ni wakulima, wafanyakazi, warina asali, wafugaji, wavuvi na maeneo mengine  ya huduma za jamii.

"UVCCM ni sehemu ya uhai wa CCM , Chama kina Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020, iliyoainisha sera za msingi na jinsi serikali  itakavyotekekeza wajibu wake katika kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano baada ya kuunda dola,"alisema.

Alisema  kwa muktadha huo, UVCCM inajiona ina dhima na wajibu wa awali katika kubeba jukumu la ama kuikosoa serikali isiporidhisha au kuisifu na kuitia ari, ikiwa inakwenda sawa kulingama na matakwa ya Ilani ya Uchaguzi, hususan katika maendeleo ya kisekta.

"Tutaandamana kwa amani na utulivu  wilaya zote na  mikoa yote ili kuuhakikishia ulimwengu, kumthibitishia na kumhakikishia Rais Dk. Magufuli, tuko naye bega kwa bega, tunaridhishwa na utendaji wa serikali yake katika kutekeleza yaliyoahidiwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM,"alisema.

Kwa mujibu wa Shaka, UVCCM tayari imetoa maelekezo kwa makatibu wa umoja huo, wajumbe wa kamati za utekelezaji za wilaya na mikoa pamoja na wajumbe wa Baraza Kuu ngazi zote, kuwataka  washirikiane na kuhakikisha wanaratibu kwa uhakika ili kufanikisha maandamano hayo.

Alisema maandamano katika ngazi za wilaya, yataanzia kwenye ofisi za UVCCM za wilaya na kumalizikia kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya huku ya mikoa yakianzia ofisi za UVCCM mkoa na kumalizikia ofisi ya mkuu wa mkoa husika.

Pia, alisema makatibu wote wa wilaya na mikoa wa UVCCM, kuanzia kesho wametakiwa kutuma maombi polisi ngazi husika ama wilaya au mikoa  ili kupata vibali kisheria, kupatiwa ulinzi na hatimaye kufanikisha maandamano hayo.

"Ikitokea polisi hawatakubali kuyaruhusu maandamano yetu yasifanyike katika wilaya au mkoa, UVCCM watalazimika kuandamana kwa kujilinda wenyewe kwa nia ya kufikisha ujumbe tunaokusudia kwa rais, serikali na dunia nzima,"alisema.

Alisema wana matumaini kuwa polisi wataruhusu maandamano hayo  kwa kuwa si maandamano yasiyo na ukomo, hayana nia ya kuleta ghasia au vurugu,  bali yana azma ya  kuhamasisha na kuijengea matumaini serikali ili iendelee kutimiza wajibu wake.

Shaka alisema vijana wote wa UVCCM, wananchi, wapenzi wa amani na utulivu, wanakaribishwa kushiriki katika maandamano hayo na hawatazuiliwa kwa sababu ama za kisiasa au kiitikadi, kwa kuwa dhamira ni kuwasilisha ujumbe wa pamoja wenyewe manufaa na tija endelevu kwa nchi na kuhimiza maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

No comments:

Post a Comment