Tuesday 23 August 2016

VIGOGO NIDA WAOMBA DHAMANA MAHAKAMA KUU



VIGOGO sita wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakidaiwa kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi  sh. bilioni moja, wamewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Vigogo hao, akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo, Dickson Maimu, wanakabiliwa na kesi hiyo, ikiwa na mashitaka 27, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, waliwasilisha maombi hayo  Mahakama Kuu, Ijumaa iliyopita.

Maimu na wenzake hao, ambao walifikishwa Mahakama ya Kisutu, Jumatano, iliyopita na wako rumande kutokana na mahakama hiyo, kutokuwa na mamlaka ya kutoa dhamana, waliwasilisha maombi hayo kwa  kupitia jopo la mawakili wanaowatetea katika kesi hiyo,  Michael  Ngalo, Seni Malimi, Audax Kahendaguza, Sylvester Kakobe, Gordian Njaala, Godwin Nyaisa.

Hatua ya vigogo hao kuwasilisha maombi hayo, inatokana na Mahakama ya Kisutu, kutokuwa na mamlaka ya kutoa dhamana na kusikiliza shauri hilo, kutokana na  Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kutoipatia kibali cha kusikiliza shauri hilo na kiwango cha fedha kilichoko katika hati ya mashitaka kuzidi sh. milioni 10, hivyo kutakiwa kuwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu.

Mbali na Maimu, waombaji wengine wa dhamana ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Maimu na wenzake wamewasilisha maombi hayo yakiambatana na hati ya kiapo, ambacho muapaji ni Wakili Ngalo kwa niaba ya wenzake, ambapo wanaiomba Mahakama Kuu kuwapatia dhamana kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Aidha, wakili huyo anadai waleta maombi wana wadhamini wa kuaminika, ambao watahakikisha wanafika mahakamani kila wanapohitajika.

Pia, anadai waleta maombi walikamatwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na polisi na waliachiwa kwa dhamana, wana makazi Dar es Salaam na familia zao, ambazo zinawategemea na walionyesha ushirikiano kwa wapelelezi kuhusiana na mashitaka yanayowakabili.

Jumatano iliyopita, Maimu na wenzake saba, walifikishwa Mahakama ya Kisutu na TAKUKURU, wakikabiliwa na kesi hiyo, ambapo hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa, alidai hawana pingamizi kuhusu dhamana ila washitakiwa wanatakiwa kuwasilisha maombi Mahakama Kuu, kutokana na kiwango kilichotajwa katika hati ya mashitaka kuzidi sh.milioni 10.

Hata hivyo, kati ya washitakiwa hao wanane, mawakili wa utetezi akiwemo Jamhuri Jonson, wanaowawakilisha Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Meneja Biashara, Avelin Momburi, waliomba Mahakama ya Kisutu, kuwapatia dhamana kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayaangukii chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Ombi hilo lilipingwa na Wakili Mbagwa, akidai kuwa washitakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi bila ya kuangalia shitaka linaangukia chini ya kifungu gani cha sheria, wanapaswa kuomba dhamana Mahakama Kuu.

Baada ya kusikiliza hoja hizo Ijumaa iliyopita, Hakimu Mwijage alitoa uamuzi juu ya maombi ya dhamana kwa Makani na Momburi, ambapo alikubali kuwapatia dhamana na kuwapa masharti, yakiwemo  kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili, watakaowasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya sh. milioni 200 na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika. Kesi hiyo ya msingi imepangwa kutajwa Agosti 19, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Maimu na wenzake wanakabiliwa na  mashitaka ya kutumia madaraka vibaya, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri, kusababisha hasara ya sh. 1,169,352,931 na kula njama.

No comments:

Post a Comment