Tuesday 23 August 2016

DK MWAKYEMBE AZIONYA ASASI ZA KIRAIA

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amezitaka asasi za kiraia nchini kutoyumbishwa na misaada kutoka nje yenye kukinzana na mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.

Alitoa ushauri huo jana, mjini Dar es Salaam, alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP).

Aidha, alisema serikali inaunga mkono juhudi za asasi za kiraia za kuelimisha jamii na kutetea haki za watoto, wazee, wanawake, walemavu na makundi mengine maalumu.

Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alisema serikali haitazivumilia asasi ambazo zinaenda kinyume na maadili ya nchi na kukiuka sheria na taratibu ambazo nchi imejiwekea.

“Serikali inaunga mkono kazi zinazofanywa na asasi za kiraia nchini, lakini niweke wazi hatutazivumilia asasi zinazoyumbishwa kwa misaada kutoka nje na kujihusisha na vitendo, ambavyo vinakiuka maadili, kanuni na taratibu za nchi, ambazo zipo kwa mujibu wa sheria,” alisema Dk. Mwakyembe.

Akitolea mfano wa mashinikizo hayo kutoka kwa nchi zenye nguvu kiuchumi duniani ya kuzitaka nchi zinazoendelea au asasi zikubali ushoga na ndoa za jinsia moja kama sehemu ya haki za binadamu ili ziweze kuendelea kupata misaada kutoka kwao.

“Asasi zenye mwelekeo huu nchini, zitachunguzwa na zitakazobinika zitachukuliwa hatua kali,” alisema Dk. Mwakyembe.

Aliongeza: "Nchi hizo zimekuwa zikitoa shinikizo kwa nchi zetu na hasa asasi nyingi, zikizitaka zikubali ushoga na ndoa za jinsia moja.
Tunazichunguza asasi zote za kiraia zenye mwelekeo huo na tukibaini mapungufu hayo, tutazichukulia hatua kali za kisheria. Uchafu na upuuzi huo wa wazungu, ubaki huko huko kwao."

Dk. Mwakyembe alisema iwapo nchi italegeza kamba katika suala hilo, baadaye itashinikizwa hata kufunga ndoa na wanyama wa kufugwa kwa madai kuwa ni sehemu ya haki za binadamu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Amon Mpanju, aliziomba asasi za kiraia kuisaidia serikali kupeleka ujumbe sahihi wenye mafundisho kwenye jamii kuliko kusubiri kukosoa.

“Tunazitaka asasi za kiraia kuacha kuunga mkono hoja za ushoga kwa kishawishi cha fedha wanazopewa kutoka kwa wafadhili wao,” alisema Mpanju.

No comments:

Post a Comment