Tuesday 23 August 2016

CUF YAMEGUKA


BUNDI ameendelea kutawala ndani ya chama cha Civic United Front (CUF), ambapo sasa kimekumbwa na mgawanyiko mkubwa wa makundi mawili.

Mgawanyiko huo unahusisha kundi kutoka upande wa Tanzania Bara,  ambalo kwa kiasi kikubwa linamuunga mkono Profesa Ibrahim Lupumba na lile la visiwani, linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, ambaye anatuhumiwa kuchochea mgawanyiko huo.

Hali hiyo ilijidhihirisha wazi baada ya baadhi ya viongozi na walinzi wa chama hicho chenye makao makuu yake, Buguruni, Dar es Salaam,  kuwazuia wajumbe wa mkutano mkuu kutoka Tanzania Bara, kuingia kwenye ofisi hizo.

Mvutano huo ulizuka baada ya baadhi ya viongozi wa CUF, akiwemo Maalim Seif, kudaiwa kutoa maagizo hayo kwa kudai wajumbe kutoka Tanzania Bara na baadhi kutoka Zanzibar, walihusika kufanya vurugu kwenye mkutano mkuu wa chama hicho, uliofanyika juzi, Dar es Salaam, kwa kutaka kurudishwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti Profesa  Lipumba.

HAMAD RASHID ALONGA,
AIBUA MENGINE MAZITO

Aidha, miongoni mwa waanzilishi wa CUF, Hamad Rashid Mohamed, ameweka bayana kiburi, tabia ya kuendekeza visasi na kutojali misingi ya kidemokrasia, kunakofanywa na Maalim Seif kuwa ndiko kumesababisha chama hicho kumeguka.

Hamad Rashid, ambaye ni Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), alitaja mambo sita yaliyosababisha chama hicho kupasuka vipande viwili.

“Kwanza tukio la vurugu kwenye mkutano mkuu limeashiria aina ya uongozi uliopo ndani ya CUF. Ni uongozi usiozingatia misingi ya demokrasia kwa chama kuongozwa na mtu mmoja (Maalim Seif).

“Mpasuko huo, Maalim Seif, ndiye aliyeuchochea kwa sababu kwenye uchaguzi wa viongozi wa CUF, ambao katibu mkuu ndiye msimamizi, maeneo yote ya Zanzibar yalipiga kura, lakini wilaya saba za Tanzania Bara, uchaguzi haukufanyika.

“Alifanya hivyo kwa sababu upande wa pili wanampinga kutokana na udikteta wake ndani ya chama,” alisisitiza Hamad.

Alisema hila hizo za Maalim Seif, zimetokana na tabia ya kung’ang’ania madaraka kwa muda mrefu huku akikiongoza chama hicho kwa misingi ya uhasama na visasi.

“Maalim Seif ni mtu wa visasi na chama hakiwezi kuongozwa na mtu wa aina hiyo, kwani hata kwenye msiba wa aliyekuwa Rais wa awamu ya pili wa Zanzibar, marehemu Aboud Jumbe, licha ya kukataa kumpa mkono Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, hata mimi nilipomfuata kumpa mkono alikataa.

“Kiburi chake na tabia ya kuendekeza visasi, watu wa Zanzibar wamefanya vizuri kutompa kura kwani ameshindwa kuimarisha amani na usalama wa chama, Je, angeweza kuimarisha amani nje ya chama?” Gwiji  huyo wa masuala ya siasa na demokrasia alihoji.

Aliongeza kuwa, Maalim Seif, amekidhalilisha chama hicho kwa kwenda kinyume na katiba, hivyo wanachama wa CUF wamepata funzo kwa tabia ya ubinafsi na uchu wa madaraka aliokuwa nao Maalim Seif.

HALI TETE MAKAO MAKUU 

Idadi kubwa ya wajumbe wa mkutano mkuu, jana, walikusanyika nje ya makao makuu ya chama hicho, yaliyoko Buguruni, ili kufahamu hatma ya mkutano huo, lakini walizuiwa kuingia kwenye ofisi hizo kwa madai kuwa, wanaotaka Lipumba aendelee kuwepo ndani ya chama hicho, hawatoruhusiwa.

Baadhi ya wajumbe waliozuiliwa kuingia, walisema mkutano huo ulivunjika kwa sababu ya ukiritimba wa Katibu Mkuu, Maalim Seif.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Julius Magoiga, alisema walifika kwenye ofisi hizo kufahamu hatma kuhusu yaliyotokea kwenye mkutano mkuu na kudai nauli, lakini walikutana na hali ya kushangaza.

Alidai alipofika ofisini hapo, alielezwa kuwa wajumbe kutoka bara hawaruhusiwi kuingia makao makuu ya chama hicho kwa madai ya kuwa vinara wa kushinikiza Profesa Lipumba, kurejea kwenye chama hicho.

“Lengo letu kufika katika ofisi za makao makuu ya chama ni kutafuta usuluhishi wa mambo, ambayo yalisababisha kuvunjika kwa mkutano mkuu juzi, pamoja na kudai nauli zetu, lakini tumezuiwa kuingia.

"Huu ni mpango mchafu, ambao unafanywa na Maalim Seif, ambaye anatumika na Edward Lowassa, kwa ajili ya kuiua CUF na mbinu zake zimebainika, hatutakubali,” alisisitiza.

Katibu wa chama hicho wilaya ya Geita, Severine Magese, alisema watakwenda kuwaeleza wanachama kile ambacho kimetokea kwenye mkutano huo na kuwasisitizia kwamba, Mwenyekiti wa CUF ni Profesa Lipumba.

“Tutawaleza jinsi ambavyo baadhi ya viongozi wakubwa wa chama akiwemo, Maalimu Seif, wanavyotumika kuua chama,” aliongeza.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CUF Wilaya ya Kahama, Mwinyi Salumu, alisema ukiritimba unaofanywa na Maalim Seif ni tamaa ya madaraka aliyokuwa nayo kiongozi huyo.

Alieleza kuwa juzi, kwenye mkutano mkuu, Maalim Seif, hakutaka Profesa Lipumba, apewe nafasi ya kujieleza kipi kilichomfanya kujiuzulu na sababu ya kutaka kurejea tena kwenye wadhifa huo.

“Katiba ya chama inaeleza wazi kuwa, mhusika anapaswa kujitetea ili utetezi wake ujadiliwe, lakini Profesa  Lipumba alinyimwa haki yake ya msingi kutokana na shinikizo la Maalim Seif.

“Tutaendelea kumtambua Lipumba kama mwenyekiti wetu wa chama na kama Wanzanzibar hawamtaki, wabaki na Seif wao, sisi hatumtambui,” Salum alitoa kauli hiyo iliyoashiria mpasuko wa pande mbili ndani ya chama hicho.

WANASIASA WAFUNGUKA

Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuia ya Wazazi,  Mzee Ali Haji Ali, alisema kuzuka  ghasia, ugomvi hadi watu kuchapana ngumi katika  mkutano mkuu wa CUF, ni kielelzo cha  uchanga wa vyama vya upinzani, kukosekana nidhamu, uwazi na ukandamizaji  wa misingi ya demokrasia.

Alisema kilichotokea kwenye mkutano mkuu wa chama hicho ni fedheha na aibu kwa viongozi wake, kwa sababu hamkani na ghasia zile zingeweza hata kupoteza maisha ya watu.

Mzee Ali alitoa matamshi hayo jana, mjini Unguja, kufuatia kuzuka fujo na tafrani kubwa, ambazo zimesababisha mkutano wa chama hicho kuvunjika katika mazingira hatarishi kabla ya kuokolewa na FFU.

Alisema chama cha siasa ambacho kitafikiria kuwa  na viongozi wa kudumu kwa miaka mingi, wasiotaka kupisha wenzao, kina hatari ya kukawia kupata mageuzi ya kifikra na kimfumo na sio rahisi kujiepusha na kadhia ya mivutano.

Akizungumzia kinachoendelea ndani ya chama hicho, Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa CUF (Bara), Julius Mtatiro, alisema  wanachotazama ni jambo moja tu la kujaza nafasi zilizo wazi.

Mtatiro alisema suala la Profesa Lipumba, limemalizika kwa kuwa mkutano mkuu umepiga kura na asilimia kubwa kuridhia asirudishwe kwenye wadhifa huo.

Alisema hali inayoendelea sasa ni ya muda kutokana na wakati na kwamba, baada ya siku kadhaa mambo yatakaa sawa na kila mmoja kuendelea na shughuli zake.

"Suala la Profesa Lipumba limemalizika, mkutano umeamua asirudishwe kwenye nafasi yake. Maamuzi ya wengi yataheshimiwa ila kwa sasa tunachoangalia ni jinsi ya kujaza nafasi zilizo wazi,"alisema.

No comments:

Post a Comment