Tuesday 23 August 2016
MAJALIWA AWAONYA WATENDAJI KUTOGUSA FEDHA ZA MAENDELEO
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa halmashauri mkoani Katavi, kuwa makini na matumizi ya fedha za maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao na atakayethubutu kuzichezea zitamuunguza.
“Fedha hii tafadhali ni ya moto. Hii ni kwa ajili ya wananchi, itawaunguza vidole msicheze nayo."
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi, wakati akihutubia umati mkubwa wa wananchi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kiwanja cha Azimio, wilayani Mpanda.
Alisema serikali imeanza kupeleka fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali, hivyo ni vema kila mtendaji ahakikishe zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi iliyokusudiwa na si vinginevyo.
Waziri Mkuu alisema ni lazima wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wahakikishe viwango vya ubora wa miradi inayojengwa katika maeneo yao inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwenda wilayani Mpanda na kuangalia namna ya kuipanua Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, ambayo inahudumia mkoa wote wa Katavi.
Alisema hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1957, kama zahanati ambayo kwa sasa inatumika kutoa huduma kwa wananchi wote wa mkoa huo jambo lililoifanya izidiwe, hivyo alimuagiza mkuu wa mkoa huo, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga kuharakisha ujenzi wa hospitali ya mkoa.
Aidha, Waziri Mkuu alisema wakati mkoa ukiwa kwenye harakati za ujenzi wa hospitali ya mkoa, wilaya nazo zianze ujenzi wa hospitali za wilaya ili kuhakikisha sera ya serikali ya kuwa na hospitali katika kila wilaya inatekelezwa.
Alisema kwa sasa madaktari na wauguzi wanaofanya kazi kwenye hospitali ya Manispaa ya Mpanda, wamezidiwa kutokana na kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa kuliko uwezo wao. Aliwaomba madaktari na wauguzi hao kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzao wa manispaa.
Hospitali hiyo kwa sasa ipo chini ya Manispaa ya Mpanda, hivyo Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa mkoa huo kuboresha huduma kwa kupeleka dawa na vifaa tiba vitakavyoiwezesha kuhudumia wagonjwa wa mkoa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment