Tuesday 23 August 2016
WATUHUMIWA 27 WA KUCHOMA MOTO MABWENI MBARONI
POLISI mkoa wa Arusha wanawashikilia watuhumiwa 27, kutokana na matukio ya kuchoma moto shule sita katika mkoa wa Arusha kwa kipindi cha wiki tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema watuhimiwa hao ni pamoja na walimu, wanafunzi, walinzi wa shule na baadhi ya wananchi.
Mkumbo alisema walimu wanaoshikiliwa, hawajahusika na matukio ya uchomaji moto moja kwa moja, isipokuwa wanatuhumiwa kushindwa kusimamia kikamilifu nyadhifa walizopewa katika shule.
Alisema katika tukio la shule ya sekondari, watu watatu wanashikiliwa akiwemo mwalimu wa zamu, mlinzi na mwalimu wa bweni huku shule ya sekondari ya Nanja, watu watatu wanashikiliwa, akiwemo mlinzi na walimu wawili.
Mkumbo aliongeza kuwa, katika shule ya sekondari ya Ole Sokoine, baadhi ya walimu wanashikiliwa pamoja na wanafunzi, ambao walionekana wakikimbia kutoka katika chanzo cha moto huo.
Aidha, kwa shule ya sekondari ya Longido, walinzi watatu, mwalimu wa zamu na mwanafunzi, ambaye alikuwa amepewa adhabu ya kurudi nyumbani kwa muda, pia wanashikiliwa huku mwanafunzi mmoja akisakwa na polisi.
Katika hatua nyingine, jengo la utawala katika shule binafsi ya Winning Spirit, limeteketea kwa moto baada ya mwalimu, ambaye jina lake linahifadhiwa, kulala katika moja ya ofisi hizo bila kutoa taarifa kwa uongozi.
Akithibitisha kuungua kwa jengo hilo, Kamanda Mkumbo alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa nane usiku, wakati wanafunzi wa bweni wakiwa wamelala.
Mkumbo alisema muda mfupi kabla ya jengo hilo kuungua, wanafunzi wawili, ambao hakuwataja majina yao, walionekana wakirandaranda nje bila sababu za msingi.
Alisema baada ya nusu saa, jengo la utawala lilianza kuungua na ndipo ikabainika kuwa kuna mwalimu alilala katika moja ya ofisi hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment