Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli akihutubia maelfu ya wananchi waliofurika kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, wakati wa mkutano wa kampeni |
Dk. Magufuli akisisitiza jambo wakati wa mkutano huo. |
Wananchi wakimshangilia Dk. Magufuli alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa |
Mgombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini, Frederick Mwakalebela, akiomba kura kwa wananchi wakati wa mkutano huo |
Dk. Magufuli akimtambulisha mfanyabiashara, Salim Abri Asas kwa wananchi wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Samora |
NA WAANDISHI WETU
MGOMBEA urais wa CCM, Dk John Magufuli, ameendelea
kuwatia tumbo joto watendaji wa serikali wenye kujilimbikizia mali, kuendekeza
vitendo vya rushwa na ufisadi kwa kuwatangazia kiama pindi atakapochaguliwa
kuwa rais.
Dk. Magufuli amesema viongozi wa serikali wenye
kuendekeza semina, kujilimbikizia fedha huku magari yao wakiyajaza mafuta saa
24 wakati wafanyakazi wa kada ya chini na wananchi wakiteseka, atawashughulikia
na hawatompenda kamwe.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika kwa wingi
kwenye Uwanja wa michezo wa Samora mjini Iringa jana, Dk. Magufuli alisema
kwenye serikali yake wafanyakazi wavivu wakatafute kazi ya kufanya.
Katika hotuba yake, ambayo Dk Magufuli alitumia saa 1:05
huku akishangiliwa na wananchi hao, alisema wafanyakazi wachache wamejinufaisha
kwa fedha za rushwa na ufisadi.
Alisema wafanyakazi watakaobainika kufanya vitendo vya
ubadhirifu wakatafute kazi zingine nje ya utumishi wa uuma kwani, kwenye
serikali yake hatokuwa na nafasi kwa wezi, wabadhirifu na wazembe.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa maslahi na mazingira mazuri
kwa watumishi wa umma watakaotimiza wajibu wa kuwatumikia Watanzania,
yataangaliwa kwa jicho la pekee ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ari kubwa.
“Najua kuna wengine wanaharibu eneo moja na kisha
wanahamishiwa kwenye ofisi nyingine. Sasa nawaambia wafanyakazi wa aina hiyo kwangu
hawatokuwa na nafasi, wakatafute kazi za kufanya na ninafahamu watanichukia,”
alisisitiza Dk Magufuli kwa sauti ya ujasiri.
Alisema wafanyakazi wachapakazi wajiandae kupata maslahi
mazuri kwa kuboreshewa mishahara yao kama alivyofanya kwenye idara alizokuwa
akiziongoza katika Wizara ya Ujenzi.
Dk. Magufuli alibainisha kuwa kutokana na uchapakazi mzuri
wa wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wafanyakazi wengi
wanavutiwa kufanyakazi kwenye taasisi hiyo kutokana na kuwepo kwa maslahi
mazuri.
“Sio kweli kuwa nitawabana wafanyakazi wasilipwe vizuri
kama baadhi ya watu wanavyodai, leo hii watu wanatamani kufanya kazi TANROADS
kutokana na maslahi mazuri yaliyokuwepo pale… kama ningekuwa hivyo kama wanavyodai
si wangekimbia kufanyakazi?” Alisema Magufuli.
Katika kuthibitisha kauli hiyo, alisema serikali imeanza
kupitia upya mfumo wa ulipaji mishahara kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha
kila mfanyakazi analipwa mshahara unaoendana na hali halisi ya maisha.
Aliwataka wafanyakazi kumpigia kura ili akapambane na
viongozi wao wanaowabana kwa kujilimbikizia mali wakati wao wakiishi kwenye
mazingira magumu.
Wananchi waliofurika kwenye uwanja huo walizizima kwa
furaha na vifijo baada ya mgombea huyo wa urais wa CCM, kumtaka mwekezaji
aliyepewa kiwanda cha usagishaji mkoani hapa, kuhakikisha kiwanda hicho
kinafanyakazi kabla ya Oktoba 25.
“Nimepita nikaona kiwanda cha National Milling kimekufa.
Sasa namtaka mwekezaji akifufue kabla sijachaguliwa kuwa rais Oktoba 25,
akishindwa aandae nyaraka za kukirudisha serikalini tukifufue,” alisema
Magufuli.
Alisema wananchi wa mkoa wa Iringa wamechoshwa kuona
kiwanda kilichobinafsishwa hakiendelezwi, hivyo kiwanda hicho kitatafutiwa
mwekezaji mwingine au kukabidhiwa vijana wa vyuo vikuu wakisimamie.
Alibainisha kuwa pindi atakapochaguliwa, serikali yake
imepanga kutengeneza ajira asilimia 9.9 hadi 40, hivyo ajira hizo zinahitaji
uwepo wa viwanda vitakavyofanyakazi.
Alisisitiza kuwa mizengwe kwa wawekezaji wenye nia ya
kujenga viwanda itaondolewa ili nchi iwe na idadi kubwa ya viwanda
vitakavyozalisha ajira kwa wingi.
“Kwenye serikali yangu kama kuna mwekezaji anayetaka
kujenga viwanda aje, hakutakuwa na njoo leo au kesho. Kama awe waziri au
mtendaji yeyote atakayeendekeza mizengwe hiyo, atatangulia yeye,” aliongeza Dk
Magufuli huku akishangiliwa na wananchi waliofurika kumsikiliza.
Aliwaeleza wananchi wa Iringa kuwa, serikali yake
itajenga uwanja wa ndege wa mkoa huo kwa kiwango cha lami, sambamba na ujenzi
wa barabara kutoka katikati ya mji huo
kwenda Tumaini ili kuondoa msongamano.
Dk. Magufuli alisema katika hatua ya kumaliza tatizo la
ajira kwa wahitimu wa vyuo vikuu, serikali yake itawakopesha wahitimu fedha za
kuanzisha miradi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment