Monday, 28 September 2015
HOMA YA BONDE LA UFA, EL-NINO KUTIKISA NCHINI
NA MARIAM MZIWANDA
WATANZANIA wametakiwa kuanza kuchukua tahadhari kutokana na taarifa za kutokea kwa Homa ya Bonde la Ufa nchini.
Ugonjwa huo hatari umetajwa unaweza kutokea tena kati ya mwezi Oktoba hadi Desemba, mwaka huu, na hiyo inasababishwa na mvua kubwa za El nino zinazotarajiwa kuanza muda wowote.
Kwa mara ya mwisho ugonjwa huo ulitokea nchini mwaka 2007 na kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na wanyama.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela, alisema mjini Dar es Salaam jana, kuwa utabiri wa hali ya hewa umebaini tishio hilo.
Amewataka Watanzania kuanza kuchukua hatua kuhusiana na ugonjwa huo pamoja na mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha.
“Kuna mvua kubwa za El nino zitatokea katika kipindi cha karibuni kuanzia Oktoba hadi Desemba, mwaka huu, mvua hizo zitasababisha madhara makubwa kwa binadamu na miundombinu. Homa ya Bonde la Ufa ni miongoni mwa magonjwa yatakayoibuka,” alisema Dk. Mwele.
Alisema taarifa za Mamlaka ya Bahari na Hali ya Hewa Marekani na Ofisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza, zote zimethibitsha kuwa mvua hizo zitakuwa na madhara makubwa kwenye maeneo mengi kuliko ilivyowahi kutokea.
Aidha, alisema Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania na Kenya, zimeshatoa tahadhari ya uwezekano wa kutokea kwa mvua za El nino na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari mapema.
Tayari Manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke, Dar es Salaam, zimewataka wananchi waishio kwenye maeneo hatarishi kuhama mara moja ili kuepuka madhara ya mvua hizo.
“Hapa nchini mvua hiyo inatarajiwa kuwepo kwenye maeneo yote ambayo yana misimu miwili ya mvua na baadhi ya maeneo yenye msimu mmoja kwa mwaka. Mvua hizo zitaambatana na mafuriko makubwa na mlipuko wa magonjwa hasa ya kuambukiza ikiwemo Homa ya Bonde la Ufa,” alisema.
Dk. Mwele alisema ugonjwa huo ni hatari na kwamba, Watanzania wengi wapo hatarini kutokana na kuambukizwa kwa mbu au kula nyama na mazao mengine kama maziwa na damu kutoka kwa wanyama ambao wameambukizwa ugonjwa huo.
“Kuna kuambikizwa ugonjwa huo kwa kugusana na mnyama aliyeambukizwa au mazao huku mbu aina ya Aedes akiwa ni chanzo cha awali na aina ya Culex na Abnopheles pia wanaweza kuwa chanzo cha maambukizo hayo,” alisema.
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa za ghafla, mafua, kutokwa na damu katika sehemu za mwili zilizo wazi, kuchanganyikiwa na kupoteza uwezo wa kuona vizuri.
Alisema ni muhimu hatua za haraka kuchukuliwa ikiwemo kufanya uchunguzi wa uwepo wa viini kinga na chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi kwenye maeneo yote yenye hatari ya mlipuko.
Dk. Mwele alisisitiza ufuatiliaji wa taarifa za hali ya hewa na uwezekano wa kutokea mafuriko uimarishwe na kutoa viashiria vya mlipuko katika maeneo mbalimbali huku wizara husika zikitakiwa kuratibu ufuatiliaji wa matukio ya ugonjwa na jinsi ya kupambana na maambukizi hayo.
Alisema ipo haja matokeo ya uchunguzi wa maambukizi kufanywa kabla ya kutoa kibali kwa wale wanaotaka kusafirisha mifugo, utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo kuwapo viuatilifu vyenye uwezo wa kuangamiza vidudu na kamati za maafa za mikoa na wilaya kutoa elimu ya kuepuka ugonjwa huo.
“Wananchi wapewe elimu kuhusu umuhimu wa kuhakikisha nyama inakaguliwa na inapikwa na kuiva, maziwa yanachemshwa kabla ya kutumiwa na kuepuka kula mizoga na yote iharibiwe chini ya uangalizi wa maofisa na jamii ya wafugaji waelimishwe kuhusu dalili za ugonjwa huo,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment