Monday 28 September 2015

DK. SHEIN AAHIDI KUFA NA MAFISADI, ASEMA VITA DHIDI YAO VITAIMARISHWA




NA MWANDISHI WETU
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, ameahidi endapo atapewa ridhaa ya kuongoza tena, atahakikisha vita dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi vinaimarishwa.
Akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni huko Mkokotoni katika jimbo la uchaguzi la Tumbatu, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Dk. Sheni alisema miaka mitano iliyopita, serikali iliweka misingi ya kusimamia utawala bora, ikiwemo kuunda taasisi mpya na kuimarisha zilizokuwepo.
Alisema katika kipindi kijacho ataweka mkazo katika kuhakikisha vyombo hivyo vinatimiza wajibu wake kwa kutekeleza na kusimamia majukumu yao ipasavyo.
“Tutapambana na rushwa na uhujumu uchumi na tutahakikisha viongozi wanatekeleza kwa vitendo maadili ya uongozi kama yalivyoelezwa kisheria, alisema Dk. Shein.
Mgombea huyo aliahidi pia kuimarisha vikosi vya Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kuvipatia vifaa na nyenzo muhimu na za kisasa zitakazowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi.
“Lengo ni kuziwezesha Idara hizi kufanya kazi kama vinavyofanya vyombo vingine vya ulinzi na usalama  nchini na kwamba sitabadili muundo wake kwa kuwa nimeridhika na utendaji wao, alisisitiza.
Alisema vikosi vya idara hizo kwa kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vimefanya kazi nzuri ya kulinda amani na kuleta utulivu nchini.
Pia, Dk. Shein aliwataka viongozi wa CUF kuacha kutumia lugha zenye kuchochea vurugu katika mikutano yao.
Alitolea mfano kauli ya kusema “safari hii CCM wakitaka wasitake watatoa serikali” na “CUF tutaipeleka serikali Mtendeni (makao makuu yao)”, ambazo zilitolewa na viongozi wa chama hicho wakati wa mkutano wao uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alifafanua kuwa kauli za namna hiyo si za kidemokrasia na kwamba hazimsaidii mwananchi kufanya uamuzi  badala yake zinatoa vitisho kwao.
Aliwakumbusha viongozi wa CUF kuwa wakiwa washirika katika serikali wanapaswa kuwa mbele katika kutii sheria.
“Sote CCM na CUF tumo katika serikali ambayo inaongozwa kwa katiba na sheria hivyo hatuna budi tuwe mfano wa kutii katiba na sheria,” alibainisha Dk. Shein.
Dk. Shein aliahidi kuendelea kusimamia amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi na kutahadharisha kuwa hakuna mtu wala kikundi kinachoweza kuzuia uchaguzi kufanyika.
Aliwaomba wananchi wamchague tena yeye  na wagombea wengine wa CCM  ili aendelee kuongoza na kuendelea kushirikiana nao kuijenga Zanzibar.
Dk. Shein alisema kuichagua CCM ni kujihakikishia amani na utulivu na kubainisha kuwa, Chama hicho  kitahakikisha kinaendelea kuimarisha mazingira mazuri yatakayowawezesha wananchi kuimarisha mshikamano wao na udugu wao.
“Hakuna mbadala wa amani, serikali nitakayoiongoza kama ilivyofanya kipindi kinachomalizika, itasimamia amani na usalama wetu ipasavyo, alisema Dk. Shein 
Alisema mwaka 2010, aliahidi akichaguliwa angejenga bandari ya kisiwa cha Tumbatu, ahadi ambayo imeshatekelezwa kwa asilimia 80 hivi sasa na itakamilika si muda mrefu.
Alisema ahadi ya kuimarisha huduma za jamii imetekelezwa kwa kiwango kikubwa na kutolea mfano huduma za afya, maji na umeme.


No comments:

Post a Comment