Na John Kiroboto
KUNA usemi kwamba katika mashindano
asiyekubali kushindwa huwa daima si mshindani na kwamba katika mashindano
mathalan ya mpira wa miguu kuna matokeo matatu; kushinda, kushindwa na kutoka
sare.
Mwaka huu Tanzania iko kwenye
kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, ambapo Oktoba 25, watakuwa wakipiga kura
kuchagua Rais, wabunge na madiwani ambapo heka heka za kampeni zinaendelea
sehemu zote nchini, huku macho yakielekezwa kwa wagombea wa CCM (Dk John
Magufuli) na wa CHADEMA (Edward Lowassa).
Sambamba na kampeni hizo, zipo taasisi
ambazo nazo zinaendesha utafiti ili kuona mwelekeo wa nchi kisiasa, lakini hasa
kutambua hisia za wananchi katika kuamua ni chama kipi na mtu gani wanadhani
wanaweza kumchagua kuongoza awamu ya tano ya uongozi wa Taifa.
Hivi karibuni, taasisi ya Twaweza
ilitoa matokeo ya utafiti wake ambao ulionyesha kuwa asilimia 62 ya wananchi
wanasema wanajisikia kuwa karibu zaidi na CCM kuliko vyama vingine.
Na hata walipoulizwa watachagua
wagombea wa chama gani – bila kutajiwa majina ya wagombea – sita kati ya 10
walisema watachagua wagombea wa CCM kwa urais (66%), ubunge (60%) na udiwani
(60%). Hivyo kutoa picha kwamba CCM inaungwa mkono.
CHADEMA kwa upande mwingine ikaonekana
kuwa chama cha pili kinachopendwa kuliko vyama vingine vya upinzani ingawa kwa
mujibu wa utafiti huo, wananchi wanaosema watachagua wagombea wa chama hicho
kwa nafasi hizo wamepungua kidogo.
Upo uwezekano kuwa wananchi
wanaopenda zaidi Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) waliunga mkono vyama vya
CUF, NCCR-Mageuzi au NLD, ingawa chama cha ACT-Wazalendo kilitajwa na zaidi ya
asilimia moja ya wananchi.
“Walipoombwa kutaja moja kwa moja jina
la mgombea urais ambaye wangemchagua, asilimia 65 ya wananchi walimtaja mgombea
wa CCM, Magufuli, asilimia 25 mgombea wa CHADEMA (na UKAWA), Lowassa na
asilimia 10 iliyosalia iligawanyika kati ya waliomtaja mmoja miongoni mwa wagombea
urais wengine, waliokataa kujibu na waliokuwa bado hawana mgombea
waliyempendelea,” ilisema taarifa ya utafiti huo.
Taarifa ilisema wahojiwa vijana zaidi,
wasomi zaidi, wanaume na wakazi wa mijini, walimuunga mkono Lowassa. Makundi ya
wahojiwa wazee zaidi, waliokuwa na elimu ya msingi tu, wanawake na wakazi wa
vijijini walielekea kumuunga mkono zaidi Magufuli.
“Hata hivyo, katika makundi yote haya,
Magufuli anaonekana kuongoza. Kwa mfano, asilimia 33 ya wananchi wenye umri wa
miaka 18 – 29 na asilimia 30 ya wenye umri wa miaka 30 – 39 wanamuunga mkono
Lowassa, tofauti na asilimia 15 ya wenye umri zaidi ya miaka 50.
“Pamoja na hayo, asilimia 57 ya wenye
umri wa miaka 18 – 29 na asilimia 76 ya wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga
mkono Magufuli. Upande wa makazi, asilimia 28 wa mijini walimuunga mkono
Lowassa tofauti na asilimia 24 wa vijijini. Asilimia 66 ya wa vijijini na
asilimia 61 ya wa mijini wanamuunga mkono Magufuli,” ilisema taarifa.
Hata hivyo, utafiti ulibaini kuwa
wananchi hawana taarifa sahihi juu ya nafasi rasmi ya UKAWA kama mseto.
Asilimia 49 wanafikiri UKAWA ni chama cha siasa kilichosajiliwa, kinyume na
hali halisi.
“Asilimia 57 wanafikiri kwamba ‘UKAWA’
litakuwepo kwenye karatasi za kupigia kura. Hii pia, si kweli. Bila kampeni na
juhudi za kuwaelimisha wapiga kura ili wawe na taarifa sahihi kuhusu jambo
hili, hali hii inaweza kuleta wasiwasi siku ya uchaguzi,” ilitanabaisha taarifa
ya Twaweza.
Utafiti
mwingine ulifanywa na Kampuni ya Ipsos (Synovate), ambao ulionyesha kwamba
mgombea wa CCM, Magufuli atashinda kwa asilimia 62 dhidi ya asilimia 31 za
Lowassa, endapo Uchaguzi Mkuu wa Tanzania ungefanyika sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti huo,
mgombea wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira angepata asilimia 0.3 huku asilimia saba
ya wapiga kura wakiwa hawajui watampigia mgombea yupi miongoni mwa wagombea wa
urais kwenye uchaguzi ujao.
Katika sifa mahususi za wagombea urais;
Dk Magufuli alionekana kuaminika zaidi katika eneo la miundombinu, ambako
asilimia 44 ya waliohojiwa walisema wanaamini atafanya mambo makubwa kwenye
eneo hilo huku asilimia 26 wakiamini Lowassa anaweza kufanya hivyo.
Lowassa alionekana kumzidi Dk. Magufuli
katika vita dhidi ya rushwa, ambapo asilimia 27 ya waliohojiwa walisema ataweza
kupambana na tatizo hilo huku asilimia 26 wakisema Magufuli atafanya hivyo.
Kuhusu ukaribu na vyama vya siasa,
waliosema wako karibu na CCM walikuwa asilimia 60, huku asilimia 29 wakisema
wako karibu na CHADEMA, asilimia tatu na CUF huku asilimia moja wakisema wako
karibu na NCCR-Mageuzi.
Kwa upande wa jinsia, Magufuli
alionekana kukubalika na wanaume kwa asilimia 51 huku Lowassa akiwa na asilimia
37, lakini kwa upande wa wanawake, Magufuli anapendwa na asilimia 69 ya
waliohojiwa huku asilimia 21 wakimpenda Lowassa.
Kama ilivyokuwa kwa utafiti wa Twaweza,
Lowassa alionekana kuwa kivutio cha wenye elimu ya juu na wakazi wa mijini,
huku Magufuli akipendwa na wa vijijini pamoja na wenye elimu ya wastani.
Kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi
nchini, ilitarajiwa kuwa utafiti huu wa Ipsos ungekuwa wa mwisho kabla ya
kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25. Sheria haziruhusu utafiti wa kisiasa
kufanyika na kutangazwa katika muda wa ndani ya siku 30 kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Lakini hivi karibuni, ikaibuka taasisi
nyingine inayojulikana kama TADIP, ambayo ni taasisi isiyokuwa ya kiserikali
iliyosajiliwa mwaka 2006, miongoni mwa shughuli kuu za taasisi hiyo ni utafiti
na ushawishi wa sera na sheria nchini.
Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi hiyo,
chini ya Mkurugenzi wake, George Shumbusho, wananchi waliulizwa ni
mgombea yupi wangemchagua kuwa rais ikiwa uchaguzi ungefanyika siku ambayo
taarifa za utafiti huu zilipokuwa zinakusanywa (wiki tatu za mwanzo, Septemba).
“Asilimia 54.5 ya washiriki walijibu
kwamba wangemchagua Lowassa, asilimia 40 Dk. Magufuli huku asilimia mbili
wakimchagua Anna Mghwira wa ACT-Maendeleo,” ilisema taarifa.
Wengine kwa mujibu wa taarifa hiyo ni
Hashimu Rungwe (0.4%) na Chief Yemba (0.1%) huku asilimia tatu wakisema hawajui
wangemchagua nani.
“Lowassa anaungwa mkono zaidi mikoa ya
Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Dar es Salaam huku Dk. Magufuli akikubalika
zaidi katika mikoa ya Dodoma na Morogoro,” ilisema taarifa. Utafiti wa mikoa
minne kwa miwili!
Kwa upande wa makundi ya umri, Lowassa
anaonekana kuungwa mkono zaidi na vijana na watu wenye umri wa kati (miaka 18-
47), watu wazima wenye umri juu ya miaka 47 wanamuunga mkono zaidi Dk.
Magufuli, ilisema taarifa.
Baada ya Twaweza na Ipsos kutoka na
matokeo ambayo moja kwa moja yalionyesha wananchi wakimpenda zaidi Magufuli,
malalamiko kutoka kambi ya UKAWA yalihanikiza kupitia vyombo vya habari na
mikusanyiko mbalimbali ikiwamo mikutano ya kampeni.
Viongozi wa UKAWA akiwamo mgombea wa CHADEMA,
Lowassa anayeungwa mkono na vyama washirika wa umoja huo na wapambe wao akiwamo
Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na wenyeviti wenza wa UKAWA, Freeman Mbowe
na James Mbatia, walisema utafiti huo ni hadaa.
Si siri kuwa matokeo ya taasisi hizo
mbili yaliwashitua na kuwanyong’onyeza kutokana na kuegemeza imani yao kwenye
‘nyomi’ za hadhira kwenye mikutano ya hadhara, wakiamini kuwa hata ukifanyika
utafiti ni dhahiri Lowassa angeibuka kidedea.
Ili kujifuta machozi kutokana na
kilichoonekana ushindi wa CCM wa mabao 2-0, wakatafuta mshambuliaji wa haraka
haraka ili angalau kuwawezesha kupata bao la kufuta machozi, ndipo TADIP
akaingia na kufanikiwa kupata bao hilo katika kipindi cha lala salama.
TADIP ilianzishwa ndani ya Chadema
mwaka 2006, chini ya ukurugenzi wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho,
Zitto Kabwe ili kufanya kazi maalumu kwa maelekezo ya chama hicho, tena chini
ya ufadhili wa shirika la Ujerumani la Konrad Adenour Foundation (KAS).
Ni TADIP hii hii ambayo Mei na
Juni mwaka huu, iliifanyia CHADEMA utafiti kujua nani ni nani kati ya
aliyetarajiwa kuwa mgombea wake, Dk Wilbrod Slaa na aliyekuwa akijitaja ndani
ya CCM, Lowassa, ambapo Dk Slaa alipewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea.
Baada ya matokeo ya TADIP, watu wa
upande wa pili na wasio na upande wakaibuka na hoja za kujua taasisi hii
ilikuwa inaegemea upande gani, ndipo nao wakakubaliana na dhana ya kutaka
kujipatia bao la kufuta machozi kwa kumwomba Shumbusho azikabili Ipsos na
Twaweza ili kuweka mambo tambarare ndani ya UKAWA.
Wakasema Shumbusho ni kada wa CHADEMA
na kutoa picha zake kwenye mitandao ya kijamii akiwa na skafu ya CHADEMA huku
akionyesha ishara ya chama hicho ya vidole viwili, ingawa katika hali ya
kutapatapa na kujitetea, mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo, Dk Joseph Mugasa
alidai picha ile ilichezewa na kuwa Shumbusho ni shabiki wa klabu ya Chelsea ya
Uingereza na alikuwa na skafu ya klabu hiyo.
Mugasa hakujisumbua hata kujiuliza kama
alama ya vidole viwili ni ya Chelsea au la! Kama si kada wa CHADEMA humo TADIP
anafanya nini huku ikijulikana kuwa ni taasisi iliyoundwa mahsusi na chama
hicho kwa kazi maalumu? Ni lini alitangaza kujiondoa CHADEMA? Sawa tukubali tu
kuwa mechi imemalizika kwa ushindi wa CCM dhidi ya UKAWA kwa mabao 2-1.
No comments:
Post a Comment