Monday, 28 September 2015

DK. BILAL AONGOZA WANANCHI KUMUAGA CELINA KOMBANI





VILIO na simanzi jana vilitawala viwanja wa Karimjee, Dar es Salaam, wakati mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, ulipowasili kwa ajili ya ndugu na jamaa kutoa heshima za mwisho.
Utulivu ulioambatana na vilio vya kwikwi ulitawala wakati gari maalumu lililobeba mwili wake lilipokuwa likiingia kwenye viwanja hivyo.
Ilipofika saa tano asubuhi, shughuli ya kuaga mwili ilianza huku viongozi wa juu wa serikali, wanasiasa na viongozi wa Chama wakiungana na Watanzania wengine kushiriki tukio hilo.
Baada ya shughuli hiyo kukamilika, baadhi ya viongozi wa serikali, wakiwemo mawaziri walimwelezea Celina kama hazina kubwa ya taifa iliyopotea wakati bado mchango wake unahitajika.
Wengi walimuelezea kuwa alikuwa kiongozi muadilifu, mchapakazi, mnyenyekevu, msikivu na mwenye ushirikiano na watu wote.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema Celina alikuwa mchapakazi hodari na mwenye misimamo, hasa linapokuja suala la maslahi kwa taifa.
“Celina alikuwa msimamizi mzuri wa sekta ya Utumishi wa Umma alipokuwa waziri na tulishuhudia mabadiliko makubwa. Alilalamikia sana suala la mishahara hewa ya watumishi ambapo alitumia ujuzi wake na kulipunguza kwa kiasi kikubwa,” alisema Makinda.
Katibu wa NEC ya CCM, Uchumi na Fedha, Zakia Meghji, alisema Chama kimepata pigo kwa kuwa Celina alikuwa kiongozi makini na hodari na muda wote alikuwa tayari kutetea wananchi wake.
“Aliwatetea kwa dhati wananchi wake na alikuwa mlezi wao na mtu wa msaada sana kwa wenye shida. Chama kinatoa pole kwa familia na wote walioguswa na msiba huu. Mungu amlaze pema,” alisema.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema serikali imepoteza mtu muhimu na mfano wa kuigwa katika uwajibikaji.
“Kila alikopelekwa alifanya kazi vizuri na kwa bidii kama Dk. Magufuli (John). Aliingia serikalini mapema hivyo nilimchukulia kama mmoja wa washauri wangu wazuri, kila ninapokwama alikuwa akinisaidia haraka,” alisema.
Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa alisema: “Alikuwa mfano mzuri kwa wanawake kutokana na kupenda kujielimisha na kujitoa kuendeleza nchi. Hata mimi nilipenda kufuata mfano wake. Hakika taifa limepata pengo kubwa, namuombea apumzike salama.”
Aliwashauri Watanzania kujenga mazoea ya kupima afya kila mara kama inavyoshauriwa na madaktari kwa kuwa magonjwa mengine hayajionyeshi haraka. Alisema Celina alionekana mzima kumbe alishaathiriwa na saratani.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, alisema aliwahi kuwa Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), huku Celina akiwa naibu wake na ndipo alipomfahamu vizuri kwamba alijitoa kwa akili zote, ujuzi wote huku akiwa na nidhamu kubwa.
“Alifanya kazi kubwa na kwa ushirikiano. Alikuwa karibu na wafanyakazi wote, hakuwa mnafiki, akijali watu wa matabaka yote. Hakika alikuwa mahiri sana katika menejimenti ya utumishi wa umma,” alisema.
Anna Abdallah, alisema enzi za uhai wake, Celina hakuwa akijivuna pindi alipoombwa ushauri, alichukulia cheo kama jambo la kawaida, alimsaidia mambo mengi hivyo ni mfano mzuri wa kuigwa katika maisha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, alisema pengo aliloancha Celina haliwezi kuzibika kwa kuwa alitoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi.
Kuzaliwa
Akisoma wasifu wa marehemu, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma),Hab Mkwizu, alisema Celina alizaliwa Juni 19, 1959, kijijini Kisewe, Ulanga, Mkoani Morogoro.
Elimu
Alisema Celina alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kwiro, iliyoko Mahenge, Morogoro kuanzia mwaka 1968 hadi 1974.
Alijiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kilalala, kuanzia mwaka 1975 hadi 1978. Mwaka 1979/1981 alipata elimu ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Wasichana Tabora.
Elimu ya Juu
“Mwaka 1982 hadi 1985 alisoma na kuhitimu elimu ya juu katika Chuo cha Elimu ya Uongozi na Utawala (IDM) Mzumbe, Morogoro na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Uongozi na Utawala,” alisema.
Aidha, mwaka 1992/1994, alisoma na kutunukiwa shahada ya Uzamili katika fani ya uongozi katika Chuo cha Maendeleo ya Uongozi, Mzumbe.
Ajira
Aliajiriwa katika Halmashauri ya Kilosa kama Ofisa Utumishi kati ya mwaka 1985 na 1992.
Mwaka 1994-1995, aliajiriwa kuwa Meneja Raslimaliwatu katika Kiwanda cha Canvas Mill, Morogoro.
Mwaka 1995 hadi 2005, alikuwa Ofisa Tawala Mkuu, Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).
Shughuli za Siasa
Mwaka 1972 hadi 1997, alikuwa mjumbe wa TANU Youth League (TYL) NA Umoja wa Vijana CCM. 1977 alikuwa kiongozi wa halaiki mkoa wa Morogoro wakati vyama vya TANU na ASP vilipoungana na kuzaliwa CCM.
Mwaka 1984 alijiunga na CCM na kupewa kadi namba 465963 na baadae namba 88646.
Mwaka 1985-1992  alikuwa Mwenyekiti wa tawi la CCM Mapinduzi Bomani, Kilosa na 1984 hadi 1992 alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kilosa.
Mwaka 2002 hadi 2007, Celina alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM, Morogoro Mjini.
Mwaka 2003 hadi 2007 alikuwa Mlezi wa Chama, Kata ya Mwembesongo na Bigwa mjini Morogoro.
Mwaka 2003 hadi 2008, alikuwa Mwenyekiti wa UWT, Morogoro Mjini.
Mwaka 2004 alikuwa kiongozi wa kampeni ya uchaguzi Serikali za Mitaa, Morogoro Mjini kata za Mwembesongo na Bigwa.
Mmwaka 2005 hadi 2015, alikuwa Mbunge, Ulanga Mashariki na Mjumbe wa Baraza la Madiwani, Wilaya ya Ulanga.
Mwaka 2007 hadi 2012,  alikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Wilaya ya Ulanga.
Mwaka 2010 alikuwa mjumbe wa Kamati Maalumu ya Kutayarisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Agosti 15, alipendekezwa na CCM na kupitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki kupitia CCM.
Nafasi za Uongozi Serikalini
Mwaka 2006 hadi 2008, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ambapo 2008 hadi 2010 aliteuliwa kuwa waziri katika wizara hiyo.
Mwaka 2010 hadi 2012 alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria na hadi umauti unamfika alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma).
Ugonjwa
Mkwizu alisema Celina alianza kuumwa mwishoni mwa Agosti, mwaka huu, akiwa katika jimbo lake la uchaguzi, Ulanga Mashariki, Ulanga, Morogoro.
Agosti 26, mwaka huu, alilazwa katika Hospitali ya TMJ, Kinondoni, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Alisema Septemba Mosi, mwaka huu, alipelekwa nchini India na kulazwa katika Hospitali ya Andhraprasth, mjini Delhi, ambapo baada ya kuchunguzwa afya yake, aligundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya kongosho ambayo iliathiri ini lake kwa kiasi kikubwa.
Leo wananchi wa Morogoro watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, kabla ya mazishi yatakayofanyika shambani kwake, nje kidogo ya mji.
Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani.

No comments:

Post a Comment