KATIBU wa NEC, Itikadi na uenezi, Nape Nnauye,
akizungumza kwenye mkutano huo, alisema mapungufu ya CCM yalisababishwa na watu
wachache ambao leo hawapo tena ndani ya chama hicho.
Alisema wachache hao walikuwa wakifanya maovu kwenye
madaraka waliyopewa seriakalini kisha kukigeukia Chama na kukifanya kichaka cha
kujifichia, jambo lililofanya wengi kukinyooshea kidole.
Aidha, aliwaasa Watanzania kuwa Taifa halihitaji rais wa
majaribio na kwamba, ifikapo Oktoba 25, mwaka huu, wamchague Dk. Magufuli ambaye
ana nia ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli.
Alisema Dk. Magufuli ni kiongozi sahihi wa kukabidhiwa
Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kwa sababu hana kasoro ya uadilifu
kwenye miaka yake yote ya utendaji wake serikalini, tofauti na mgombea wa
CHADEMA, Edward Lowassa.
Nape alisema Lowassa anamfahamu na kwamba, alipotaka
kuwa miongoni mwa makada waonesha nia ya kutaka kuchaguliwa kuiwakilisha CCM
kwenye nafasi ya urais mwaka huu, alimwambia kutokana na historia yake ya
ufisadi asingeweza kufanikiwa.
Alisema mgombea huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa
Tanzania kwa miaka miwili na kisha kujiuzulu kwa kashfa ya zabuni ya kampuni ya
Richmond, si msafi na kila alipopewa majukumu ya uongozi serikalini, aliharibu
kwa kuhusishwa na ubadhirifu wa rasilimali fedha.
Alisema tangu Lowassa alipofika Makao Makuu ya CCM kwa mara
ya kwanza, alikuwa na tabia ya udokozi na kwamba, hata baada ya kushika
nyadhifa nyingine nje ya Chama, ikiwemo uongozi wa Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC), aliendelea na tabia zake.
Nape alisema Lowassa alipokuwa kwenye wizara mbalimbali
aliendelea kutumia vibaya madaraka aliyokuwa nayo ambapo, mfano mzuri ni
alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambako
alijilimbikizia maeneo mengi makubwa ya ardhi sehemu mbalimbali za nchi.
“Lowassa si msafi, anadanganywa na akina Mbowe ajiamini,
lakini ukweli ni hafai. Wapi kapewa majukumu bila kuharibu? Kama anabisha ajitokeze
hapa akatae hadharani. Hakuna, kote alikopita kaharibu, hivyo hatuwezi kumpa
Ikulu mtu wa aina hiyo na Watanzania msimruhusu hata kuikaribia,” alisema.
Aliongeza kuwa Lowassa ni gamba namba moja
lililokisumbua Chama kwa muda mrefu, lakini baada ya kutoka na kwenda upinzani,
CCM imetulia na usafi wake wa zamani umerejea na kipo imara kuwahudumia Watanzania
kwa kipindi kingine cha uongozi wa nchi.
“Tulitembea nchi nzima miezi 28, kukagua utekelezaji wa
ilani ya uchaguzi na sera za chama, kweli kulikuwa na sehemu hazikuwa sawa na
wananchi walituambia, rushwa, dhuluma, urasimu yote haya tumepambana nayo
hayapo,” alisema Nape.
AMSHUKIA
MSIGWA
Kuhusu Mchungaji Peter Msigwa, Nape alisema hafai
kuchaguliwa na wananchi wanapaswa kumpinga hadharani kutokana na kulamba matapishi yake.
Alisema Mchungaji Msigwa aliwahi kutamka kuwa
wanaomuunga mkono Lowassa wanapaswa kupimwa kwanza akili, lakini akabadilisha
mawazo na msimamo wake baada ya kununuliwa.
“Msigwa aligoma kumkubali Lowassa mpaka apewe ‘uji
mdomoni’, akapewa uji na mpango mzima ulifanyika hotelini na kamera
ziliwakamata na picha zipo, kama anabisha ajitokeze,” alisema Nape.
Nape alisema Msigwa aliwahi kuwataka wananchi wa Iringa
kuacha kununua bidhaa za Kampuni ya ASAS, ambayo inaongoza kwa kuwaajiri vijana
wengi wa Iringa ili wamsaidie kwenye maandamano, kitu kinachodhihirisha kuwa
hafai kuwa kiongozi.
Alisema badala ya kuwa kiongozi wa mfano kutokana na
kuwa na kofia ya dini, Msigwa amegeuka kuwa tapeli, ambaye alisababisha kambi
ya ujenzi wa barabara ya Iringa kwenda Dodoma kuhamishwa Isimani kutokana na
eneo lililopangwa kuwekwa kambi hiyo awali, kuwa mali ya mchungaji huyo kwa
ajili ya kanisa lake.
Nape alisema wana Iringa umefika wakati wa kulikomboa
jimbo na kumpa kura ya ndiyo, Fredrick Mwakalebela na kuachana na Msigwa,
ambaye ameshindwa kusimamia msimamo wa kumkataa Lowassa kukinunua chama chao
cha CHADEMA.
Kuhusu Fredrick Sumaye, ambaye naye alihama CCM kwenda
CHADEMA, Nape alisema alikuwa akimheshimu, lakini kiongozi huyo aliyewahi kuwa
Waziri Mkuu katika awamu ya tatu ya serikali, amejivua heshima kuungana na
Lowassa upinzani.
Alisema Sumaye kwa sasa amekosa hoja zaidi ya kupiga
kelele kudai wataibiwa kura Oktoba 25, mwaka huu, jambo ambalo halina ukweli
kwa sababu wanatambua hawawezi kushinda uchaguzi mkuu mbele ya CCM.
LUKUVI
ANG’AKA
Akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea Ubunge wa Jimbo
la Isimani, William Lukuvi, amewataka watendaji wa serikali wasiowajibika
kuandika barua ya kuacha kazi kabla ya Dk Magufuli hajaingia madarakani.
Alisema Dk Magufuli ni mchapakazi asiyetaka mzaha kwenye
utendaji kazi, hivyo watendaji wanaofanya kazi kwa kuwadhulumu wananchi, muda wao
wa kuacha kazi umewadia.
“Anayetaka kufanya kazi na Magufuli afahamu kwamba,
hataki mchezo. Kama kuna mtendaji anayevurunda na kujificha kwenye kivuli cha
CCM, aandike barua ya kuacha kazi kabla Magufuli hajashika madaraka,” alisisitiza.
Lukuvi, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, aliwaambia wananchi waliofurika kwenye uwanja wa Samora
kumsikiliza mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli, kuwa mtindo wa baadhi ya
watendaji kutumia madalali kuwanyanyasa wafanyabiashara ndogondogo umekwisha.
Alisema Dk. Magufuli ana uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa
kuwa ana uzoefu na utendaji kazi wake umetukuka na usiotiliwa shaka.
No comments:
Post a Comment