Sunday 16 April 2017

UVCCM: WAPINZANI NI WANASIASA MAKENGEZA


UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema iwapo upinzani hauoni wala kukiri utendaji kazi wa serikali ya Rais Dk. John Magufuli, itabidi watafutiwe miwani maalumu ili washuhudie mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo yanayoendelea kufikiwa.

Aidha, umeeleza kuwa umesikitishwa na kitendo cha baadhi ya viongozi wa upinzani, kuiponda bajeti ya serikali na kuiita bajeti hewa, wakati ina manufaa na mafanikio makubwa  ya kiuchumi kwa maslahi ya umma na maendeleo ya jamii.

Hayo yalielezwa juzi na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, baada ya  uzinduzi wa ujenzi wa reli mpya kwa kiwango cha ‘standard Guerge’ na kuzungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi kifupi cha utawala wa serikali ya awamu ya tano.

Shaka alisema madai yaliyotolewa na upinzani yakiiponda bajeti ya serikali huku mashirika ya uchumi ya kimataifa, nchi wahisani na washirika wa maendeleo wakisifu juhudi zinazochukuliwa na nchi, alisema hilo linadhihirisha kuwa Tanzania hakuna upinzani wa maana  ila kuna ubishani.

"Itoshe sasa kuthibitisha Tanzania hakuna upinzani na wapinzani wa maana, lililopo ni kundi la wapayukaji, ambao hupinga na kufanya ubishani huku wakipinga hata masuala ya msingi. Hii ni aibu, wasioona kazi na utendaji wa Dk. Mgufuli tutawapatia miwani maalumu," alisema Shaka.

Alikitaja kitendo cha serikali ya awamu ya tano, kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo kwa kipindi kifupi, kuwa hayapaswi  kupingwa, kubezwa au kukejeliwa na upinzani, jambo ambalo kwa sehemu kubwa linadhihirisha aina ya upinzani uliopo, ukiwa umepoteza maana na kutokuwa na malengo.

"Serikali ndani ya mwaka mmoja na ushee, imefufua shirika la ndege na kununua ndege mpya, inajenga viwanja vya ndege, barabara, reli, na kukusanya kodi za mapato kwa kiwango cha juu, hospitali zina dawa, inasomesha wanafunzi bure kuanzia elimu ya  msingi hadi sekondari na kumaliza tatizo la madawati,"alieleza.

Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alieleza kuwa, yapo mambo ambayo upinzani unaweza kukikosoa au kulaumu kwa nguvu ya hoja Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini sio katika mambo yanayoonekana kwa macho, ambayo msingi wake ni kuipa heshima nchi na kukuza maendeleo ya watu.

Alisema kinachofanywa na serikali ya Rais Dk. Magufuli ni kuhakikisha kero zote na malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, yanatekekezwa ipasavyo, ndiyo maana upinzani unajikita na kuzungumzia hoja dhaifu, ambazo hazina tija kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment