WAZIRI wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi, Hamad Rashid Mohamed, amesema hakuna wa kumuondoa madarakani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Hamad amesema serikali yoyote duniani huondolewa ama kwa uchaguzi au kupitia mapinduzi ya silaha, sio kwa uendeshaji wa vikao, mazungumzo au maneno ya kisiasa.
Aidha, amewataka wananchi katika visiwa vya Unguja na Pemba, kujibidisha katika shughuli zao za kila siku za uzalishaji mali, kujitafutia riziki na kupigania masuala ya maendeleo.
Hamad, aliyasema hayo jana, wakati akihojiwa katika kipindi cha Asubuhi na ZBC, kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha ZBC cha Zanzibar.
Alisema hakuna mwanya, nafasi wala njia ya kuiondoa serikali iliyowekwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia na kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria.
"Nawasihi wananchi waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali, waweke mkazo katika kujijenga kiuchumi, washirikiane na serikali iliyopo madarakani, pia kupigania maendeleo huku wakiishi kwa kuzingatia misingi ya umoja, amani na utulivu,"alisema.
Waziri huyo wa SMZ, alieleza kuwa hata chama cha ASP kiliposhiriki uchaguzi wa mwaka 1957, 1961 na 1961 huku kikiona hakuna njia ya kupata utawala, kilifanya Mapinduzi yaliyoiweka SMZ madakarani tangu mwaka 1964 hadi sasa.
"Hata Sultan Qaboos wa Oman na aliyekuwa Rais wa Libya. Muamar Gaddafi, waliwaondoa baba na wajomba zao madakarami kwa njia za mapinduzi na kushika utawala wa nchi hizo, hawakupata madaraka kwa njia za mazungumzo mezani au kwa maneno ya kisiasa,"alisema Hamad.
Akitolea mfano, alisema Zanzibar yalifanyika mazungumzo mara tatu ya kusaka miafaka ya kisiasa, ambayo haikuunda serikali hadi pale vyama vyenyewe vilipokubaliana kama lipo tatizo linalohitaji mapatano ya pamoja baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.
"Zanzibar kumefanyika uchaguzi kisheria, baadhi ya vyama na wagombea wake vikasusia, Tume ya Uchaguzi Zanzibar imemtangaza mgombea aliyeshinda kutokana na kura za wananchi, Dk. Shein ataondolewa na nani ikiwa amewekwa madarakani kisheria na kikatiba? "Alihoji mwanasiasa huyo mkongwe.
Aidha, Hamad ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha ADC , alikiri kuwepo kwa tatizo la mchanga visiwani zanzibar huku serikali ikitaka zitumike njia mbili ili kunusuru tishio la uhaba uliopo wa mchanga ili kulinda na kutunza mazingira.
Alisema njia ya kwanza ni kudhibiti utumiaji wa mchanga na kukizuia kiasi kidogo cha mchanga kilichopo, wakati ya pili ni wananchi kuanza kujenga nyumba kwa kutumia matofali yanayotengenezwa kwa utaalamu na teknolojia mpya ya kisasa.
"Hata katika majengo ya nyumba za mjerumani zilizoko Kikwajuni, Zanzibar, matofali yaliyotumika ni hydrophone, ukienda Kigamboni, Dar es Salaam , Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba kwa utaalamu huo, matofali yake hayahitaji nyumba ipakwe rangi au kupigwa plasta," alisisitiza Hamad. ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya Muungano.
Akijibu swali la watu kuanza kutumia udongo mwekundu na mawe yaliyoko Bambi, mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema njia hiyo ni hatari zaidi kwani ina athari nyingi za kimazingira, iwapo utafanyika uchimbaji mawe ya miamba inayokinga nguvu na kina cha bahari.
Alisema miamba ya mawe iliyo chini ya bahari na ardhini, ikisaidiwa na mikoko, huwa ni kinga inayodhibiti na kuhimili nguvu na kasi ya kina cha maji ya bahari yasivuke na kuingia nchi kavu na kuleta athari na madhara.
No comments:
Post a Comment