Saturday 27 August 2016

CHEYO ALAANI MAANDAMANO YA UKUTA


CHAMA cha UDP kimelaani kitendo kinachofanywa na baadhi ya wanasiasa nchini, kushinikiza mikutano isiyo na afya kwa maendeleo ya nchi, badala yake inatumika kutoa kauli zanazoashiria uvunjifu wa amani.

Kimetoa wito kwa Watanzania kupuuza maandamano ya CHADEMA, yaliyopewa jina la UKUTA, yaliyopangwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka huu, badala yake watoe nafasi kwa viongozi waliochaguliwa kikatiba kutekeleza yale waliyoahidi kwa wananchi.

Hayo yalisemwa jana, Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa UDP, John Cheyo, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa siasa nchini.

Alisema hakuna nchi yoyote duniani inayotoa uhuru usio na mipaka, hivyo kinachowatesa baadhi ya viongozi wa kisiasa hapa nchini kwa sasa ni haki.

Alisema haki hiyo ni ya kufanya mikutano ya hadhara na ya ndani na maandamano, ambapo wengi wao wamesahau lengo na madhumuni ya mikusanyiko hiyo.

Cheyo alisema wanasiasa wengi wamekuwa wakiomba vibali vya maandamano, ambayo sio ya amani kutokana na maudhui ya shughuli husika hayaendani na sheria za nchi.

"Wanasiasa wengi tumekuwa tukiomba vibali vya maandamano au mikutano, lakini ndani ya mikusanyiko hiyo tunatoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa amani.

"Kumponda Rais au mtu mwingine yeyote kwenye mikusanyiko kama hiyo ni viashiria vya uvunjifu wa amani, kutokana na ukweli kwamba sio wote watakaokubaliana na kauli hizo,"alisema.

Aidha, alisema kutokana na viashiria hivyo, ndiyo maana Rais, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, aliamua kuepusha vurugu, ambazo zinaweza kutokea kwa kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa nchini.

Mbali na hilo, Cheyo alipongeza Rais Dk. Magufuli kwa utendaji uliotukuka, ikiwemo kuboresha uchumi wa nchi kupitia wawekezaji.

Cheyo alisema Rais Magufuli amefanya mambo makubwa ndani ya nchi kwa kipindi kifupi, hivyo anapaswa kuungwa mkono na kila mtu.

Aliwataka wananchi kumpa nafasi ya kutimiza ndoto zake za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda pamoja na kuboresha maeneo mbalimbali, yakiwemo ya uwekezaji, ujenzi wa reli ya kati na suala la elimu bure.

No comments:

Post a Comment