Saturday 27 August 2016

MAJALIWA KUMWAKILISHA JPM KENYA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasili mjini Nairobi, Kenya kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Sita wa Wakuu wa Nchi wa TICAD (TICAD VI), utakaofanyika Agosti 27 hadi 28, mwaka huu.

Waziri Mkuu anahudhudia mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli.

Mara baada ya kuwasili Nairobi jana, Waziri Mkuu Majaliwa alikutana na viongozi wakuu mbalimbali wa kampuni za kibiashara kutoka Japan, ambao wamewasili kuhudhuria mkutano huo.

Miongoni mwa aliokutana na kufanya nao mazungumzo ni pamoja na Waziri Mkuu na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Chiyoda Corporation, Tadashi Izawa.

Katika mazungumzo yao, pamoja na kuangalia fursa katika sekta ya gesi nchini, kampuni hiyo imekubali kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa wataalamu wa sekta ya gesi, hususan usindikaji wa gesi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.

Izawa alimweleza Waziri Mkuu kwamba, wamefurahishwa na taarifa za ugunduzi wa gesi ya Helium nchini Tanzania na kwamba, kampuni yake ina teknolojia na uzoefu wa muda mrefu katika kutekeleza miradi ya gesi.

“Tunao uzoefu wa muda mrefu, pia tunazo teknolojia za kuendeleza sekta ya gesi, ikiwemo Helium. Kwa mfano, ujuzi wa kutenganisha gesi asilia na Helium. Tumetekeleza miradi ya namna hii nchini Qatar, ambayo kwa sasa ni ya pili kwa uzalishaji wa gesi hiyo duniani, ikitanguliwa na Marekani,”alisema.

Alisema mafunzo hayo yatafanyika kuanzia mwakani na yatalenga vijana wasiopungua 10 kutoka Tanzania, ambao wamehitimu shahada za uhandisi na kwamba, tayari wameshafanya hivyo kwa vijana wanane kutoka Msumbiji.

Kwa upande wake, Majaliwa alimshukuru Izawa kwa mpango wao wa mafunzo kwa vijana wa Kitanzania, lakini akamtaka pia waangalie uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaotoka maeneo husika yenye gesi ili wapatiwe mafunzo, ambayo yatawawezesha kumudu baadhi ya kazi kwenye viwanda vya kusindika gesi.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi Kato na kujadiliana mambo mbalimbali, yakiwemo ya nishati na miundombinu.

Katika mazungumzo hayo, Kato alimweleza Waziri Mkuu nia ya shirika hilo kuendelea kusaidia miradi ya kilimo hapa nchini, hususan katika sekta za afya, maji, kilimo na miundombinu, ambazo imekuwa ikijihusisha nazo kwa muda mrefu sasa.

Katika hatua nyingine, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mathias Chikawe, alimwomba makamu huyo wa sais kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye sekta za nishati na miundombinu ya mkoa wa Dodoma, hususan katika kipindi ambacho serkali imeamua kuhamia huko.

No comments:

Post a Comment