Sunday, 13 August 2017
MABOSI WANNE TANESCO WAPANDISHWA KWA PILATO
VIGOGO wanne wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akiwemo aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu, Robert Shemhilu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa tuhuma za uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya sh. milioni 275.
Mbali na vigogo hao, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ilimpandisha kizimbani msambazaji kutoka Kampuni ya Young Dong Electronic Co. Ltd, kujibu tuhuma hizo.
Washitakiwa hao waliofikishwa mahakamani hapo jana ni Shemhilu, Ofisa Ugavi, Harun Mattambo, Mkurugenzi wa Fedha, Lusekelo Kasanga, Mwanasheria, Godson Makia na msambazaji, Martin Simba.
Washitakiwa walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Peter, aliwasomea mashitaka mawili ya kutumia madaraka vibaya na kuisababishia serikali hasara.
Shitaka la kwanza, Shemhilu, Mattambo, Kasanga na Makia wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari na Desemba 2011, katika ofisi za TANESCO, zilizoko Ubungo, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa shirika hilo, walitumia madaraka yao vibaya kwa kufanikisha malipo kwa msambazaji Martin Simba, bila ya kufanya uhakiki.
Vitalis alidai walifanya hivyo kinyume na kifungu cha 35 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma namba 21 ya 2014, kitendo ambacho kilisababisha msambazaji huyo kupata faida.
Washitakiwa wote watano wanadaiwa kati ya Januari na Desemba, mwaka 2011, katika ofisi hizo, wakiwa waajiriwa wa shirika hilo na msambazaji huyo, waliisababishia serikali hasara ya sh. 275,040,000.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Wakili Peter alidai Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ametoa hati ya kuipa mahakama hiyo mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Washitakiwa walikana kutenda makosa hayo, ambapo wakili Peter alidai upelelezi umekamilka na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Simba alitoa masharti ya dhamana kwa kumtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili, ambao kila mmoja atatia saini dhamana ya sh. milioni 40 na mmoja kati yao awe na hati ya mali isiyohamishika.
Washitakiwa walifanikiwa kutimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 24, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment