Thursday 10 August 2017

POLISI WAMJERUHI MKE WA MWENYEKITI WA MTAA KWA RISASI

ASKARI  wa Jeshi la Polisi jijini Mwanza, wameingia kwenye kashfa ya kumjeruhi kwa kumpiga risasi kwenye mguu wa kushoto, mke wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Majengo Mapya, wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza, Editha Lucas (35).

Tukio hilo lilitokea juzi, kati ya saa 4.30 na saa 5.30 usiku, katika eneo la Miembe Giza, na kuzua taharuki kubwa kwa wananchi huku  askari hao wenye silaha za moto, wakimshambulia mwanamke huyo na kumchania nguo, baada ya kuwahoji sababu za kumshambulia kwa kipigo mumewe.

Akizungumza  na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, Mwenyekiti wa mtaa huo, Ntobi Boniphace, alisema kabla ya kupigwa, kulitokea ajali ya gari lililogonga nyumba yake wakati wakiwa wamelala na familia yake ndani ya nyumba hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema ajali hiyo ilisababisha aamke na kuwasiliana na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mabatini (OCS), kumfahamisha tukio hilo na
kuwapigia simu askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Kati Kitengo cha Usalama Barabarani, kuhusiana na tukio la ajali hiyo.

Boniphace alisema baada ya kufanya mawasiliano, alifika mkuu wa kituo cha Mabatini na kumtaka asubiri taratibu za kisheria zifanyike, kabla ya kuchukua hatua.

Hata hivyo, wakiwa eneo la tukio, dakika 45 tangu kutokea kwa ajali hiyo, walifika polisi wa doria wakiwa kwenye magari mawili tofauti, moja likiwa na namba T 245 CTW na kuhoji walipo madereva wa magari yaliyosababisha ajali hiyo.

“Askari hao ambao wote walikuwa wamelewa, walipoambiwa kwamba dereva ametoweka na ufunguo wa gari lake, wakanigeukia na kuanza kunishambulia kwa kipigo, kisha wakapiga risasi mbili hewani. Licha ya OCS kuwazuia wasifanye hivyo, hawakumtii,” alisema Ntobi.

Mwenyekiti huyo alisema askari hao waliendelea kumsurubu na hata mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Kulwa Kisura, alipoingilia kati, alipigwa huku askari hao wakiendelea kurusha risasi ovyo, kuwatisha wananchi wasikaribie eneo la tukio.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, askari hao walimshambulia mkewe kwa kipigo na kumdhalilisha, huku wakimchania mavazi yake na kubaki uchi wa nyama, kabla ya mumewe kumwingiza ndani.

"Lakini bado askari mmoja alitufuata hadi chumbani na kufyatua risasi bila kujali kwamba kulikuwa na watoto wamelala,"alisema.

Mwenyekiti huyo alisema chanzo cha kupigwa kwa mkewe ni kuwahoji sababu za kumpa kipigo yeye, wakati ndiye aliyewaita baada ya kutokea kwa tukio hilo la ajali.

Alisema kilichomsikitisha ni kwamba, waliendelea kumpa kipigo mkewe hata baada ya kukimbilia chumbani, licha ya mayowe ya wananchi waliowataka wamwache kwa kuwa alikuwa akinyonyesha mtoto mchanga.

Aliongeza kuwa baada ya kumfikisha nje, askari hao walimbeba mkewe na kumtupa ndani ya gari lao huku wakiwa wamemjeruhi kwa risasi na kuondoka naye hadi Kituo cha Polisi Kati.

Alisema baada ya kufika huko, iliamriwa mkewe apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, kwa ajili ya kupatiwa matibabu kabla ya kuhamishiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, kutokana na kuvuja damu nyingi.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema, kilichofanywa na askari hao dhidi ya raia wasio na silaha, ni ukiukwaji wa haki za binadamu, sheria za nchi na matumizi mabaya ya silaha.

“Kumshambulia mwenyekiti wa serikali ya mtaa, ambaye wanashirikiana naye kuwafichua wahalifu na kumjeruhi mkewe, ni kuwatia hofu wananchi," walisema wananchi hao.

Pia, walieleza kusikitishwa kwao kuona askari hao wakikataa kutii amri ya bosi wao, OCS, huku wakimkosakosa kwa risasi, ambayo moja ilitua kwenye friji (jokofu ), alipokuwa akiwazuia wasifanye vurugu.

Mmoja wa wafanyabiashara jirani na eneo la tukio, Farida Shaaban, alieleza kuwa wakati mke wa mwenyekiti anapigwa, askari hao walikuwa wakirusha risasi hewani kama njungu na kuwalazimu wananchi kujificha kwenye vichochoro.

“Kitendo walimchofanyia mke wa mwenyekiti ni udhalilishaji wa wazi.
Wamempiga na kumchania mavazi yake na kumwacha uchi. Mbali na kipigo hicho, pia walimjeruhi kwa risasi, Kwa kweli najisikia uchungu kwa kitendo hicho. Lazima askari hawa wachukuliwe hatua,”alisema Farida.

Baada ya tukio hilo, baadhi ya kinamama walikuwa wakingua vilio huku wakishinikiza kuandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kulalamikia vitendo hivyo.

Mwandishi wa habari hizo alishuhudia maganda 14 ya risasi, yaliyookotwa katika eneo la tukio, ingawa kuna madai kuwa, zaidi ya risasi 40 zilitumika.

Uchunguzi wa Uhuru umebaini kuwa, dereva anayedaiwa kusababisha ajali hiyo, alikuwa akinywa pombe kwenye baa iliyoko kwenye moja ya chumba cha nyumba hiyo na kusahau kuzima gari, ndipo kondakta akaenda kuligeuza, likamshinda na kuparamia ukuta.

Diwani wa Kata ya Mabatini (CHADEMA), Deo Lucas, alilaani tukio hilo, ambalo alilielezea kuwa ni la kinyama na kuahidi kushirikiana na vyombo vya  dola kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.

KAULI YA RPC

Akizungumza na Uhuru kwa simu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alikiri kuwepo kwa tukio la mtu mmoja kujeruhiwa na kuongeza kuwa, ameagiza uchunguzi ufanyike dhidi ya askari wanaotuhumiwa kushiriki ili kupata ukweli.

“Hakuna aliyekufa kwenye tukio hilo, ila kuna majeruhi. Siwezi kusema hiyo ni risasi, tunasubiri wataalamu watatupa taarifa kama ni risasi au la,"alisema na kuongeza:

"Nimeagiza askari wafanye uchunguzi ili kubaini kilichosababisha vurugu hizo hadi askari hao wakapiga risasi ovyo, ingawa inaelezwa tukio hilo lilisababishwa na ajali ya gari kuparamia na kugonga ukuta."

Alisema iwapo itabainika kuwa, askari walioshiriki kwenye tukio hilo walikuwa wamelewa, watachukuliwa hatua za kinidhamu.

No comments:

Post a Comment