Thursday, 10 August 2017

KIKWETE AONGOZA MAZISHI YA BILIONEA WA ARUSHA


RAIS mstaafu Jakaya Kikwete, ameongoza maelefu ya waombolezaji katika mazishi ya bilionea wa Arusha, Faustine Mrema (64), yaliyofanyika kwenye eneo la hoteli yake ya nyota tano ya Ngurdoto Mountain Lodge, iliyoko wilayani Arumeru, mkoani hapa.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Balozi mstaafu, David Kapya, aliyemwakilisha Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, mabalozi na wabunge

Wengine ni wafanyabiashara wakubwa wa sekta ya utalii kutoka ndani na nje ya nchi.

Mazishi hayo yalifanyika katika moja ya kumbi za hoteli hiyo, wenye uwezo wa kubeba watu 5,000, ambao ulifurika mpaka nje.

Akihubiri katika ibada ya mazishi hayo, ambayo iliongozwa na maaskofu sita, Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangelism, Dk. Eliud Issangya, alisema ni vyema kila mtu akatambua kuwa, kuna maisha ya milele ambayo Mungu amewaandalia binadamu.

Askofu Dk. Issangya alisema watu wanatakiwa kuishi kama wasafiri, badala ya kuringia utajiri mkubwa walionao.

"Katika dunia hii, sisi ni wapitaji tu, kuna maisha ya milele, ambako ndiko maisha yetu ya kudumu yaliko, hivyo ni vyema  tukaacha tabia ya utajiri tulio nao katika dunia hii kwani ni ubatili mtupu,"alisema Dk. Issangya.

Akimzungumzia Mrema, askofu huyo alisema licha ya kuwa kiongozi wake wa dini, alikuwa rafiki yake mkubwa, ambaye walishirikiana katika mambo mbalimbali ya kusaidia jamii.

RC GAMBO

Akitoa salam za pole kwa niaba ya serikali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema marehemu alikuwa chachu ya maendeleo, ambapo aliweza kujenga vitega uchumi vingi, ambavyo vilitoa ajira kwa vijana.

Kuhusu mchango wake kwa jamii, Gambo alisema alijitoa katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kuchangia maendeleo ya Arusha, kwa kusaidia ujenzi katika Hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru.

"Marehemu Mrema alikuwa kiungo muhimu katika jamii, ambapo hivi karibuni alichangia bodaboda katika mpango ulioanzishwa na ofisi yangu kwa ajili ya vijana wa Arusha," alisema Gambo.

Aliongeza kuwa, kabla ya kuondoka kwenda Afrika Kusini, alimwita na kumuomba amuongoze kwenye sala ya toba, kisha akaanza safari.

ARUSHA YASIMAMA

Wakazi wa Jiji  la la Arusha na viunga vyake, walisimamisha shughuli zao kwa saa moja, wakati mwili wa mfanyabiashara huyo maarufu katika sekta ya utalii, ukisafirishwa kutoka nyumbani kwake eneo la Uzunguni kupelekwa Ngurdoto.

Pia, wananchi walijitokeza kwa wingi kujipanga barabarani na kuupungia msafara huo, ambao uliongozwa na magari ya polisi na pikipiki maalumu.

WAFANYAKAZI WALIA

Mara baada ya mwili huo kuwasili Ngurdoto, wafanyakazi waliokuwa wamevaa nguo nyeusi na kujipanga mstari, waliangua vilio vya huzuni kuonyesha mapenzi makubwa waliyonayo kwa mkurungenzi wao.

Mrema, ambaye alikuwa na elimu ya middle school, ambayo aliipata kati ya mwaka 1961-1968, wilayani Rombo, alifika Arusha mwaka 1970 na
kujishughulisha na shughuli mbalimbali.

Mwaka 198O,  alianza kujikita kwenye biashara ya utalii, ambapo alianza ujenzi wa hoteli yake ya kwanza ya The Impala, Jijini Arusha.

Baada ya ujenzi huo, Mrema alianza kupata mafanikio makubwa, ambapo aliendelea kuwekeza katika sekta ya utalii  kwa kuanzisha Kampuni ya Classic Tours & Travel, The Impala Shuttle & Services,  Hoteli ya Naura Spring, Hoteli ya Impala katika mkoa wa  Kilimanjaro na Ngurdoto Mountain Lodge.

Mrema, ambaye hakuwa na taaluma mahususi, licha ya elimu yake ndogo,
alikuwa na kipaji cha hali ya juu cha kufanya mambo mengi makubwa kuliko wasomi wengi.

Moja ya kazi alizozifanya kwa weledi mkubwa ni pamoja na za taaluma ya uhasibu na shughuli za kibenki, bila kusomea taaluma hiyo rasmi.

Aidha, alikuwa na kipaji cha ubunifu, ujasiri, uwezo wa kuona mbele na kufanya mambo mengi makubwa kwa wakati mmoja, bila woga katika shughuli zake za ujenzi wa mahoteli na usafirishaji katika sekta ya utalii.

Pia, aliwaheshimu watumishi wasio wababaishaji na alikuwa tayari kufanya kazi na mtu yeyote, bila kujali kiwango cha elimu na taaluma yake.

Mrema alifariki wiki iliyopita katika Hosptali ya Garden City ya Afrika Kusini, alikokwenda kupatiwa matibabu na mwili wake uliletwa nchini Agosti 5, mwaka huu

No comments:

Post a Comment