Thursday, 10 August 2017

UHAMIAJI YAANZISHA MSAKO KWA WAWEKEZAJI


IDARA ya Uhamiaji nchini, imeanzisha doria nchi nzima ili kuwasaka wawekezaji wasiozingatia sheria za uhamiaji, kwa kufanyakazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.

Hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwepo na taarifa za baadhi ya wawekezaji, hasa wenye viwanda, kugeuza baadhi ya maeneo yao kuwa makazi ya wafanyakazi raia wa kigeni.

Lengo la msako huo ni kuhakikisha wawekezaji wote wanafuata sheria za uhamiani na uwekezaji nchini, kwa kutochukua nafasi za ajira zinazofanywa na Watanzania.

Akizungumza jana, Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, alisema hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kwenda kinyume cha sheria hizo.

"Hatutaki wawekezaji wababaishaji wanaochukua nafasi za ajira za Watanzania. Tutafanya doria na tunapowakamata, tunawachukulia hatua za kisheria.

"Tunapotekeleza majukumu yetu, tunahakikisha lazima sheria za nchi zinafuatwa. Hata kwa Watanzania wanaotaka kwenda nje ya nchi, lazima nao wazingatie sheria na taratibu za uhamiaji," alieleza.

Alisema hatua za kuwarejesha wahamiaji haramu kwenye nchi walizotoka, hailengi kwa baadhi ya mataifa, bali ni matakwa ya kisheria, hivyo yeyote atakayekiuka taratibu zilizowekwa, atachukuliwa hatua.

Kamishna Jenerali alieleza kuwa, kutokana na hali ya ulinzi na usalama kuzorota kwenye mataifa mbalimbali, Tanzania imekuwa ikikabiliwa na wimbi la wahamiaji haramu, ambao baadhi yao wamegundulika kufanya uhalifu.

Alisema kwa sababu hiyo, Idara ya Uhamiaji inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ulinzi na usalama wa taifa unakuwa kipaumbele muhimu.

Uchunguzi uliofanywa na Uhuru, umebaini kuwepo kwa baadhi ya wageni haramu kwenye mitaa mbalimbali hapa nchini, ambao nyakati za mchana hufungiwa ndani na kuruhusiwa kutoka nyakati za usiku kwa ajili ya kununua mahitaji yao, ikiwemo chakula.

Idara hiyo pia inaendelea na msako kwa wamiliki wa baadhi ya viwanda wenye mtindo wa kuwaficha wahamiaji haramu ndani ya viwanda vyao na kufanyakazi kinyume na sheria na kuwaomba viongozi wa mitaa kuwapa ushirikiano.

Kamishna Jenerali Dk. Anna, amewataka wamiliki wote wa viwanda wenye wageni wasio na vibali, kufuata taratibu za nchi na wakikamatwa, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa vile watakuwa wamefanya makosa.

Idara hiyo inaendelea kufanya operesheni maalum katika mikoa mbalimbali na jana, ilitarajiwa kuwafikisha mahakamani wahamiaji haramu 72, kutoka Ethiopia. Wahamiaji hao walikamatwa mkoani Pwani, wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment