Thursday, 10 August 2017

MANJI HATARINI KUFUNGULIWA KESI NYINGINEUPANDE wa Jamhuri umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuuruhusu kumchukua mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji,  anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, akahojiwe na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhusiana na masuala ya kodi.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, alikataa ombi hilo na kuutaka upande huo kutafuta utaratibu mwingine kwa kuwa faili lililoko mahakamani hapo, halihusiani na masuala ya kodi.

Hayo yalijiri mahakamani hapo jana, wakati shauri hilo linalowakabili Manji na wenzake watatu, lilipopelekwa kwa kutajwa.

Ombi hilo liliwasilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, ambaye aliiomba mahakama hiyo, mshitakiwa huyo achukuliwe na TRA kwa ajili ya kuhojiwa na angerudishwa ndani ya muda wa kazi.

Mawakili wanaomtetea Manji, wakiongozwa na Alex Mgongolwa akishirikiana na Hudson Ndusyepo na Semi Malimi, walidai ombi hilo halikuwa sahihi kwa jana.

Mgongolwa alidai kuwa mawakili wa Manji, wanaoshughulikia masuala ya kodi, walishafanya mawasiliano kwa njia ya maandishi.

“Sisi sio mawakili wa Manji wanaoshughulikia kodi, hivyo tunahitaji kuwasiliana na mawakili hao ili mahojiano yawe na manufaa,” alidai Mgongolwa na kuhoji iwapo upande wa jamhuri unamuomba Manji au kampuni zake na kwa jana, mteja wao aliwaarifu suala hilo halitawezekana.

Wakili Kishenyi alidai anayehitajika kwenye mahojiano hayo ni Manji na wala siyo kampuni zao. Aliiomba mahakama kumruhusu mshitakiwa huyo na akifika huko, iwapo ataona kuna haja ya kuwa na wataalamu wake, atasema.

Manji aliieleza mahakama kwamba, alishaanza kufanya mawasiliano na TRA, hivyo alikubaliana na maelezo ya mawakili wake.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkeha aliutaka upande wa jamhuri kutafuta utaratibu mwingine kwa kuwa mahakamani hapo, hakuna faili linalohusiana na kodi. Shauri hilo liliahirishwa hadi Agosti 18, mwaka huu, kwa kutajwa.

Mbali na Manji, washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo Meneja Rasilimali Watu, Deogratius Kisinda, mtunza stoo, Abdallah Sangey na mtunza stoo msaidizi, Thobias Fwele,  ambao wote wanasota mahabusu Gereza la Keko, kutokana na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuzuia dhamana zao.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka saba, yakiwemo ya kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mihuri ya JWTZ.

Mashitaka hayo yanayowakabili, yanaangukia chini ya Sheria za Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa, ambapo siku ya kwanza waliposomewa mashitaka hayo, Julai 5, mwaka huu, DPP, aliwasilisha hati ya kupinga wasipewe dhamana.

Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na DPP hajawasilisha hati ya kuipa mamlaka ya kusikiliza.

No comments:

Post a Comment