Tuesday 8 August 2017

SIKO TAYARI KUVUNJA KATIBA YA NCHI- JPM




RAIS Dk. John Magufuli amesema kamwe hawezi kufanya mambo, ambayo yapo kinyume cha Katiba ya nchi, ndiyo maana hawezi kuzidisha muda wa kukaa madarakani.

Pia, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, kugawa vibanda vya biashara 128, vinavyozunguka stendi ya mabasi kwa wananchi wa Korogwe, badala ya wale wanaotoka nje.

Rais Magufuli alielezea msimamo wake huo jana, baada ya Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, maarufu Profesa Maji Marefu, kuomba aongezewe miaka mingine 10, ili aweze kukaa madarakani kwa miaka 20, kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli, aliitoa wakati alipokuwa akizindua stendi mpya ya mabasi ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga.

"Mnaniombea nikae miaka mingine ili iwe 20, nilielewa kuwa mnataka niishi miaka 20, zaidi na sio miaka 20 ya urais, hilo haliwezekani kwa sababu naheshimu Katiba," alisema.

Alisema kazi ya urais ni ngumu kwa sababu anatumbua majipu mengine, ambayo yameoza na kusababisha kushindwa hata kwenda kula.

"Ni kazi ngumu, ambayo inahatarisha maisha, lakini lazima nifanye kwa niaba ya Watanzania, kwa sababu nisipotumbua, nani atakuja kufanya hivyo? Inawezekana asipatikane mwingine wa kutumbua, bora niyatumbue yote kwa sababu mimi ni jasiri wa kutumbua," alisema.

Akizungumzia ujenzi wa stendi hiyo mpya yenye maduka zaidi ya 128, ambayo imegharimu sh. bilioni nne, alisema ina uwezo wa kuingia mabasi mengi.

"Stendi hii inaweza kutumika wakati wa mvua, jua na hata usiku kwa sababu kuna taa. Nyinyi mmekuwa ni miongoni mwa wilaya 11, ambazo zimepata stendi nzuri ya kimataifa katika Tanzania nzima," alisema.

Rais Magufuli alisema maduka hayo ya biashara yanatakiwa kupangishwa na wananchi wa Korogwe, siyo vinginevyo.

"Nisije kukuta maduka haya yapo wazi au mkubwa mmoja amekataa kupangisha na anataka kupangisha ndugu zake tu, wakati hakutoa hata fedha ya kujenga hayo mabanda, yamejengwa na serikali inayoongowa na Rais Magufuli," alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliiomba TAMISEMI kusimamia hilo ili kusiwepo na vikwazo wala masharti makubwa kwa wananchi kupata maduka hayo kwa ajili ya kufanyabiashara.

"Maana kunaweza kukatafutwa watu, ambao hata hawakai Korogwe, ili wamiliki hayo maduka. Nataka hivi vibanda vyote wapewe watu wa Korogwe, kwa sababu vimejengwa Korogwe. Kama Mkurugenzi una mtu wako unataka kuja kuwapangisha, mbakishe huko huko asihangaike kuja hapa," alisema.

Pia, aliwaonya makandarasi wote watakaochelewesha miradi ya maendeleo kwamba, hatasita kuwatumbua iwapo watakwenda kinyume na makubaliano.

AWAONYA WANANCHI

Rais Magufuli aliwaonya wananchi, ambao wanashindwa kulima na kusubiria serikali iwapelekee chakula wakati wa njaa.

"Mnatakiwa kulima. Najua kuna watu watakuwa wanawacheka, lakini nyinyi fumbeni macho, fanyeni kazi. Katika maendeleo ya nchi, unapochukua hatua yoyote kuibadilisha nchi, wapingaji lazima watakuwepo tu," alisema.

Alisema wananchi wanatakiwa kufanyakazi kwa sababu serikali ya Rais Magufuli haigawi fedha za bure.

"Usipofanyakazi, hata hizo fedha ulizokuwa nazo zitapotea. Kwa hiyo mafisadi wakae wakijua hilo. Zile fedha walizokuwa wakizipata kwa wananchi maskini, hawatazipata tena na wakifanya ufisadi sasa hivi, wajiandae kutumbuliwa na kwenda jela," alisema.

ALIA NA WALIOJIMILIKISHA MASHAMBA

Alisema kuna mashamba zaidi ya 72, yalimilikiwa na watu binafsi na wengine waliyachukua kwa ajili ya kupata mikopo, lakini yatarudishwa yote kwa wananchi.

"Naomba mniamini ndugu zangu wa Korogwe, serikali tunachukua hatua na lazima tuzichukue kwa kuzingatia sheria, kwa sababu nimeapa kulinda sheria na Katiba," alisema.

Aliongeza: "Yale mashamba, ambayo hayajaendelezwa, msimamo upo pale pale, nimeshaongea na viongozi wa mkoa, walete ripoti ya mashamba yanayotakiwa kufutwa na mengine kupunguzwa."


MKANDARASI APEWA WIKI MBILI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagiza wakandarasi wanaosimamia mradi wa maji wawe katika sehemu yao ya kazi ndani ya wiki mbili, vinginevyo warudishe sh. bilioni 2.8, walizolipwa.

Pia, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, kuwakamata wakandarasi hao endapo hawatarudi kwenye eneo lao la kazi ndani ya wiki hizo, ili wakaeleze namna ya kuzirudisha fedha hizo.

Agizo hilo alilitoa jana, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Handeni, mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo. Wakandarasi hao ni Mkandarasi Mshauri, Don Consult na Mkandarasi Mjenzi,  Tansino.

Alisema fedha za Magufuli, hasa zile za serikali ya awamu ya tano, hazipotei hovyo,  hivyo lazima zirudi.

"Najua hawapo katika sehemu yao ya kazi na wameshakula fedha, wananchi wanasubiri maji, hawayaoni. Sasa ninasema leo (jana), najua wananisikia, kwa mujibu wa sheria, ninataka ndani ya wiki mbili warudi katika eneo lao la kazi. Najua walisimamishwa, sasa nataka warudi waanze kuyachimba haya mabwawa kwa fedha zao," alisema.

Aliongeza: "Kwa hiyo wachague kurudi kwenye eneo la kazi au wazirudishe hizo fedha. Naomba uongozi wa mkoa walisimamie hilo, hatuwezi Tanzania kupoteza fedha nyingi hivyo."

"Changamoto kubwa iliyopo Handeni ni maji na mji huu unakuwa kwa haraka, lakini tatizo la maji bado lipo. Lazima nikiri kuwa, changamoho hizi za maji ni nzito, lakini nimeamua kuzivalia njuga ili tusiwe na historia ya kuhangaika na maji," alisema.

Rais Magufuli alisema miaka ya nyuma, kulikuwa na miradi ya kuchimba mabwawa katika eneo la Mkata, Manga na Dungwa, iliyogharimu sh. bilioni 4.1.

Alisema mkandarasi alipewa kazi na kulipwa sh. bilioni 2.8 na zilizosalia kwa ajili ya kumalizia mradi ni sh. bilioni 1.2, lakini bado hazijatumika kwa sababu mkandarasi aliyepewa kazi hiyo alifanya hovyo.

"Akalipwa fedha nyingine, lakini kazi aliyoifanya ni ya fedha kidogo na hao waliokuwa wakimlipa wapo na wanastarehe na hizo asilimia walizopewa. Mtumbua majipu nimefika," alisema.

WABUNGE WATOA YA MOYONI

Mbunge wa Korogwe Vijijini, Majimarefu alisema katika awamu ya nne na ya tano, jimbo hilo liliahidiwa vitu vingi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya lami, lakini hadi sasa haijajengwa.

"Vilevile, tuliahidiwa kuwa Mji wa Mombo utakuwa halmashauri, lakini haujawa. Pia, tuliahidiwa bwawa kubwa la maji, ambalo litawasaidia wananchi, lakini hatujaliona," alisema.

Alisema maeneo mengi ya Korogwe yamezungukwa na mashamba ya mkonge, lakini baadhi ya viongozi wa serikali hawasemi ukweli kwa sababu, yanayoendelezwa ni machache.

"Tunaonewa sana, na sisi hatupendi kusema sema sana kwa sababu ni viongozi wa CCM. Wananchi wangu wanakuwa wanyonge kwa sababu hawana sehemu ya kufanya maendeleo," alisema.

Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, alimuomba Rais Magufuli kusonga mbele kwa sababu hakuna, ambaye atamsimamisha.

Akizungumzia changamoto za Korogwe, alisema inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, tatizo ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Pia, alimuomba Rais Magufuli awajengee kiwanda cha matunda kwa sababu kilichokuwepo kilibinafsishwa huku mwekezaji huyo aking'oa mitambo na kuondoka nayo.

"Tunaomba basi hata gofu aliloliacha utupe ili sisi tuliendeleze na kuweka vifaa ili wananchi wapate kiwanda cha kusindika matunda yao," alisema.

No comments:

Post a Comment