Tuesday, 8 August 2017

MWIJAGE AAPA KULA SAHANI MOJA NA WAWEKEZAJI FEKI


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameapa kula sahani moja na wamiliki wa viwanda vilivyobinafsisha, ambao wameshindwa kuviendeleza.

Amesema alishindwa kuitekeleza kazi hiyo kama alivyoagizwa na Rais Dk. John Magufuli, kutokana na changamoto mbalimbali alizokutana nazo, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viwanda kuwa chini ya wizara zingine na vingine kutokuwemo kwenye orodha ya viwanda vilivyobinafsishwa.

Mwijage amesema amepanga kuianza kazi hiyo Ijumaa wiki hii na kuonya kuwa, atatekeleza majukumu yake bila kuwa na maneno.

“Kuna watu wengine wameingia kwenye sekta ya viwanda, lakini hawajui shughuli yake, wengi wanang’ang’ania faida tu. Moja ya masharti ya viwanda, watu walitakiwa kuviendeleza, lakini kuanzia Ijumaa, nitaanza kutenda bila kuwa na maneno," alisema Mwijage alipohojiwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds, jana.

Mwijage alielezea msimamo wake huo siku moja baada ya Rais Dk. Magufuli kutangaza hadharani kwamba, amekuwa akimkwaza kwa kushindwa kuvirejesha viwanda vilivyobinafsishwa, ambavyo wahusika wameshindwa kuviendeleza.

Akihutubia wananchi wakati wa ufunguzi wa Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro, mjini Tanga, juzi, Rais Magufuli alisema kitendo cha waziri huyo kuwa na kigugumizi katika kutekeleza agizo hilo, kimekuwa kikimkwaza.

Rais Dk. Magufuli alisema amekuwa akimpa maelekezo Waziri Mwijage kuhusu suala hilo, ofisini kwake Ikulu, kwenye vikao vya baraza la mawaziri na katika mikutano ya hadhara, lakini haoni viwanda hivyo vikifutwa.

Alikwenda mbali zaidi kwa kusema, inaonekana waziri huyo anaogopa sura za baadhi ya watu waliobinafsishiwa viwanda hivyo na kumtaka afumbe macho na kuanza kutekeleza majukumu ya kuvichukua, ikiwa ni pamoja na kuvipiga faini kwa kuchelewesha maendeleo.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, vipo viwanda 197, ambavyo vimelala, havifanyikazi na kwa mkoa wa Tanga, vipo viwanda zaidi ya 11, vilivyokufa kabisa, lakini wahusika wanadanganya kuwa, vinafanyakazi kwa kuvipaka rangi na kuwaweka walinzi kwenye mageti.

"Kujenga viwanda sio mchezo. Yapo maelekezo ya Rais, viwanda
vilivyobinafsishwa na havitumiki, virudishwe. Rais alichokitegemea kwangu sio kile anachokiona, sababu viwanda haviendi kwa kasi anayoiona na hii kuna sababu kadhaa,” alisema Mwijage wakati wa mahojiano hayo.

“Hii sekta ya viwanda ni multi-sector, maana kuna viwanda vipo chini ya wizara ya mifugo, vingine maliasili, kuna viwanda vimechukuliwa, lakini havipo kwenye list ya viwanda vilivyobinafsishwa, nahitaji wakuu wa mikoa waingie hapa,” alisema Waziri Mwijage

Aliongeza kuwa, kwa suala la kiwanda cha Mang’ula, tayari mgogoro wake umefika bungeni na mmiliki wake ameitwa na bunge kuhojiwa.

Waziri huyo alisema kwa kiwanda cha matairi cha Arusha, kimeongezewa nguvu, lakini serikali bado inahitaji mwekezaji atakayekuwa na nguvu zaidi kwenye uzalishaji.

“Kiwanda cha General Tyre kina historia kubwa zaidi. Kilikuwa cha Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini sasa ni mali yetu. Siwezi kumsemea mheshimiwa Rais, najua ana imani na mimi, ndio maana nilimuomba asinikumbushe tena siku nyingine,” alisema na kusisitiza waziri huyo.

Akitoa mfano mwingine, Waziri Mwijage alisema kiwanda cha Mgololo cha Mufindi, kinafanyakazi, lakini kuna baadhi ya shughuli nyingine za uzalishaji zinaendelea nje ya nchi.

Kwa mujibu wa sheria ya ubinafsishaji, mwekezaji ambaye hajakiendeleza kiwanda katika kipindi cha miaka 20, atanyang'anywa kwa kushindwa kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment