Tuesday, 8 August 2017

MANJI AKWAMA MAHAKAMA KUU, OMBI LAKE LA DHAMANA LATUPWA


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya dhamana yaliyokuwa yamewasilishwa na mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji, baada ya mawakili wake kuyakubali mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na upande wa jamhuri.

Hata hivyo, kabla ya kutupiliwa mbali kwa maombi hayo, Manji aliieleza mahakama kwamba, hataki Wakili Peter Kibatala kumwakilisha kwa sababu za kisiasa na hakumpa maelekezo ya kufanya hivyo.

Hayo yalijiri jana, mahakamani hapo, mbele ya Jaji Isaya Arufani, wakati maombi hayo ya dhamana ya Manji, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, yalipopelekwa kwa kusikilizwa.

Manji aliieleza mahakama kuwa, alipopeleka maombi ya dhamana, alimpa maelekezo Wakili Joseph Thadayo, hata hivyo alishangaa siku yalipopelekwa kwa kusikilizwa, alikuja Wakili Kibatala kumwakilisha.

Mfanyabiashara hiyo aliieleza mahakama kuwa, hataki Kibatala amwakilishe kwa sababu za kisiasa na kwamba, atakuwa akiwakilishwa na mawakili Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Seni Malimi, ambao walikuwepo mahakamani hapo.

Baada ya Manji kueleza hayo, upande wa jamhuri, ambao ulikuwa ukiwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Simon Wankyo, walidai wamewasilisha mahakamani hapo hati ya kiapo kinzani na mapingamizi ya awali.

Kadushi aliomba kabla ya kusikilizwa kwa maombi ya Manji, yasikilizwe mapingamizi yao ya awali.

Wakili wa Manji, Mgongolwa alidai maombi ya dhamana ya mteja wao yana dosari na kwamba, wanakubaliana na mapingamizi ya awali ya upande wa jamhuri kwa kuwa yana msingi. Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Kadushi, aliiomba mahakama kuyatupilia mbali maombi hayo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote husika, Jaji Arufani alitoa amri ndogo, ambazo ni Manji kutowakilishwa na Wakili Kibatala kwa sababu za kisiasa na maombi hayo ya dhamana kuyatupilia mbali kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuyasikiliza.

Akifafanua baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili Kadushi alidai Manji, ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, alipaswa kuwasilisha maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Uhujumu Uchumi na Rushwa.

Manji (41), yupo mahabusu kwenye Gereza la Keko, tangu Julai, mwaka huu, baada ya kusomewa mashitaka, yakiwemo ya kukutwa na vitambaa vya kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana yake na wenzake watatu.

Mshitakiwa huyo aliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu, akiiomba , itengue hati ya kupinga dhamana yake, iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP). Pia anaiomba mahakama hiyo iridhie kumpatia dhamana kwa sababu ana matatizo ya kiafya, anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Katika maombi yake hayo, Manji aliambatanisha na vyeti vya daktari kuhusu matatizo yake ya kiafya.

Hata hivyo, baada ya kuwasilisha maombi hayo, DPP ambaye ni mlalamikiwa kwenye maombi hayo, aliwasilisha hati ya kiapo kinzani na mapingamizi ya awali yakiwa na sababu tatu, ambazo ni mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo, vifungu vya sheria vilivyotumika kuyawasilisha siyo sahihi na hati ya kiapo iliyoambatanishwa kuyaunga mkono yana dosari, ambazo hazirekebishiki.

Manji na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi  ya msingi katika Mahakama ya  Kisutu, ambapo baada ya kusomewa mashitaka, DPP aliwasilisha hati ya kupinga dhamana zao.

Mbali na  Manji, washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Meneja Rasilimali Watu, Deogratius Kisinda (28), mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na mtunza stoo msaidizi, Thobias Fwele (43).

Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashitaka saba yakiwemo ya kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mihuri ya JWTZ.

Mashitaka hayo yanayowakabili, yanaangukia chini ya Sheria za Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa, ambapo siku ya kwanza waliposomewa mashitaka hayo, Julai 5, mwaka huu, DPP aliwasilisha hati ya kupinga wasipewe dhamana.

Washitakiwa hao walisomewa mashitaka hayo wakiwa katika wodi namba moja ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, iliyoko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya mahakama kuamua kuhamia hospitalini hapo kwa ajili ya kumsomea mashitaka Manji, aliyekuwa amelazwa.

Kutokana na hali hiyo, washitakiwa wenzake watatu nao ilibidi wapelekwe hospitalini hapo wakitokea kituo cha polisi ili waweze kusomewa mashitaka pamoja.

Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na DPP hajawasilisha hati ya kuipa mamlaka ya kusikiliza.

Upande wa jamhuri uliwasilisha hati ya kupinga dhamana ya DPP, ambapo ilipingwa na mawakili wa washitakiwa hao, hivyo kuifanya mahakama itoe uamuzi kwamba, haiwezi kuzungumza lolote kuhusu hilo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Manji na wenzake wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya Chang’ombe ‘A’, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na ofisa wa Polisi wakiwa na mabando 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za jeshi hilo, zenye thamani ya sh. milioni 192.5, ambavyo vilipatikana isivyo halali.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa Julai mosi, mwaka huu, katika maeneo hayo, walikutwa na ofisa wa polisi, wakiwa na mabando manane ya vitambaa hivyo vyenye thamani ya sh. milioni 44.

Shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maandishi 'MKUU WA KIKOSI 121 KIKOSI CHA JESHI JWTZ',  bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Washitakiwa hao wanadaiwa siku hiyo, walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maneno 'KAMANDA KIKOSI 834 KJ MAKUTUPORA DODOMA,' bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Manji na wenzake, pia wanadaiwa siku hiyo walikutwa na mhuri mwingine wenye maneno 'COMANDING OFFICER 835 KJ, MGAMBO P.O BOX 224 KOROGWE.'

Washitakiwa hao wanadaiwa Julai mosi, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na vibao vya namba za usajili za magari vyenye namba SU 383 na SM 8573, ambavyo vilipatikana isivyo halali.

No comments:

Post a Comment