Sunday 6 August 2017

MAALIM SEIF AMEFILISIKA KIFIKRA- SAKAYA



NAIBU Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya, amesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Seif Sharrif Hamad, ameanza kufilisika kifikra.

Amesema ameshangazwa na hatua aliyochukua kiongozi huyo, kuwasilisha barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francsi Mutungi, kutaka kuwavua uanachama wabunge wawili, akiwemo yeye na Maftaha Nachuma (Mtwara).

Naibu Katibu huyo alisema, Hamad hana mamlaka ya kumng'oa uanachama kutokana na kuwa ni kinyume na katiba na kwamba, Baraza Kuu la Taifa la chama hicho ndilo lenye mamlaka hayo.

"Katiba yetu ibara ya 91 (C) inataka vikao vyote vya baraza kuu viongozwe na mwenyekiti wa chama, hivyo hakuna kikao cha baraza kilichoongozwa na mwenyekiti,"alifafanua.

Magdalena alisema hawezi kukubali kuonewa na Katibu Mkuu huyo na kwamba, vikao walivyokaa ni batili, hivyo hiyo ni dalili kwamba, amekwishaanza kufilisika kifikra.

Aliongeza kuwa Maalim Seif amekuwa akiwadanganya wabunge ambao wamefukuzwa uanachama kuwa, atawatetea wakati kufanya hivyo ni kuwaponza na kuwadanganya.

"Kutokana na mgogoro huu unavyoendelea, watu wengi ambao sio wanachama, wamekuwa wakisoma katiba na wameniambia kuwa ni kweli Hamad anakiuka katiba ya chama,"alisema.

Aliongeza kuwa haiwezekani Hamad kumfukuza uanachama na kwamba, anachokifanya ni kuufurahisha umma na wafuasi wake bila kutambua kuwa anajidhalilisha.

Katika hatua nyingine, chama cha Alliance For Democratic Change  (ADC), kimemtaka Maalim Seif akubali kukaa na Mwenyekiti wake, Profesa Lipumba ili kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo.

Pia, kimemtaka mwanasiasa huyo aheshimu maamuzi ya Msajili wa Vyama vya Siasa au ajiondoe kwa heshima kwenye ulingo wa siasa na kuwapisha viongozi  wengine.

Kimesema suluhisho pekee lenye nusura na yeye kisiasa siyo kuendelea kufukuza wanachama wenzake, wakiwemo waasisi wa chama hicho, akiwemo Mussa Haji Kombo na Nassor Seif Amour, kwa sababu amefukuza wengi na hajafanikiwa.

Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa ADC Taifa, Hamad Rashid Mohamed,  alipozungumza na Uhuru, mwishoni mwa wiki, kwenye makao makuu ya chama hicho, Bububu, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Hamad alisema kuna kila dalili na ishara zinazooonyesha kuwa, Maalim Seif amepoteza uwezo wa kuendelea kukiongoza chama chake, hivyo  busara pekee ni kujiondoa kwenye siasa na kuwaacha vijana kukiendesha  na yeye abaki kama mtazamaji na mzee wa busara.

Alisema ukaidi, ubishi au kutaka kupimana misuli na msajili wa vyama vya siasa ili kutaka maamuzi yake yawe sahihi kuliko matakwa ya kikatiba au kufukuza wenzake kila siku, hakutamsaidia kwa kuwa ameshawafukuza wengi na hajaambulia lolote.

"Namshauri akubali kufanya mojawapo kati ya mambo matatu, akubali kukaa chini na mwenyekiti wake, aheshimu ushauri wa msajili wa vyama vya siasa au ajiondoe kwa heshima katika uwanja wa siasa na kuwaachia wengine,"alisema Hamad.

Alisema chama cha siasa kinahitaji kuendeshwa kwa mkusanyiko wa fikra mpya, mawazo mbadala, mpangilio wa dira na mipango makakati kulingana na mahitaji ya nyakati, badala ya umimi, ubishi au ukaidi.

"Kibri kwetu waumini wa kiislam ni nguo ya Mungu, sifa ya kibri sio nzuri kulinganishwa nayo  binadamu (mahluku). Binadamu mzuri hukubali majadiliano, mazungumzo na maafiikiano. Ukaidi na ubishi ni nyenzo za kubomoa, sio za kujenga jambo likawa,"alisema.

Hamad alisema yanayotokea sasa ndani ya CUF ni matokeo ya ubishi na kutoambilika kwa Maalim Seif, kwani aliwahi kumshauri wakati ilipoundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, abaki serikalini na chama kiongozwe na wengine, lakini akapinga.

Mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, alisema hakuna jambo jema kwa kiongozi kama kutazama maslahi mapana ya taasisi anayoiongoza na pia kuishi kwa kuheshimu katiba na utaratibu.

No comments:

Post a Comment