Sunday 6 August 2017

JPM AMCHANA LAIVU MWIJAGE

RAIS Dk. John Magufuli amemweleza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk.Charles Mwijage, kwamba amekuwa akimkwaza kwa kushindwa kuvirejesha viwanda vilivyobinafishwa, ambavyo wahusika wameshindwa kuviendeleza.

Dk. Magufuli amesema kitendo cha waziri huyo kuwa na kigugumizi katika kutekeleza agizo hilo, ambalo amekuwa akimpatia mara kwa mara kwenye vikao na hata ofisini kwake, limekuwa likimkwaza.

Alisema ameshangazwa kuona Waziri Mwijage anaogopa kutekeleza agizo hilo, ikilinganishwa na utekelezaji unaofanywa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wa kufuta mashamba makubwa yasiyoendelezwa.

Rais Dk. Magufuli amesema amekuwa akimpa maelekezo Mwijage kuhusu suala hilo ofisini kwake, kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri na hata katika mikutano ya hadhara, lakini haoni viwanda hivyo vikifutwa.

Aliyasema hayo jana, wakati wa ufunguzi wa Kiwanda cha Saruji cha Kilimanjaro, ambapo alisema hajui kitu gani kinachomfanya waziri huyo kuogopa kuvifuta viwanda wakati Lukuvi amekuwa akifuta mashamba makubwa na kumkabidhi ripoti.

"Bado sijaona viwanda vilivyofutwa na mimi ndilo ninalotaka kuliona. Sijui ni kitu gani kinachomfanya kuogopa. Nataka kuona viwanda vyote ambavyo vimeshindwa kuendelezwa, vinachukuliwa na serikali, "alisema.

Aliongeza kuwa inaonekana waziri huyo anaogopa sura za baadhi ya watu waliobinafsishiwa viwanda hivyo.

"Nataka kuona watu wananyang'anywa viwanda hivyo bila kuogopa sura ya mtu ama kiongozi yeyote na kwamba, haijalishi anayefutiwa ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) CUF au CHADEMA,"alisisitiza.

Rais Dk. Magufuli alisema sheria ya ubinafsishaji inafafanua kuwa, mwekezaji ambaye hajakiendeleza kiwanda katika kipindi cha miaka 20, anyang'anywe hivyo ni jukumu la Waziri Mwijage kutekeleza agizo hilo.

Alisema jambo ambalo linasikitisha ni kuona kuwa, wapo baadhi ya watu walitumia fursa hiyo ya ubinafsishaji, kukopa fedha kwenye benki na kufungua miradi mingine, huku viwanda vikiachwa kuwa ghala la kuhifadhia bidhaa.

"Inasikitisha sana kuona baadhi ya wawekezaji hao, wamefikia hatua ya kuchukua vifaa vya viwanda hivyo na kuviuza nje ya nchi. Mbali na hilo, wapo waliochukua viwanda hivyo na kuviuza kama maghala kwa matajiri,"alisema.

Alisema hatua iliyochukuliwa na serikali kuingia kwenye ubinafsishaji, ilikuwa na lengo zuri, lakini wawekezaji hao walichukua viwanda hivyo kwa bei ya kutupa na kutumia fursa hiyo kukopea mikopo benki kwa ajili ya miradi mingine.

Alimtaka Waziri Mwijage kufumba macho na kuanza kutekeleza majukumu ya kuchukua viwanda  hivyo na kwamba, ikiwezekana kuvipiga faini ya kuchelewesha maendeleo. 

"Kwa miaka yote hiyo 20, hawakufanya hivyo na wamewakosesha fursa za ajira Watanzania na mapato ya serikali, kwa hiyo lazima virudishwe wapewe watu ambao wana lengo la kuviendesha,"alisema Rais Magufuli.

Alisema vipo viwanda 197, ambavyo vimelala, havifanyi kazi na kwa mkoa wa
Tanga, vipo viwanda zaidi ya 11, vilivyokufa kabisa na kwamba, wahusika wanadanganya kuwa vinafanya kazi kwa kuvipaka rangi na kuwaweka walinzi katika mageti ili ifahamike vinafanyakazi.

Rais Dk. Magufuli alisema kuna haja ya kujiuliza ni wapi palipokosewa katika suala la ubinafsishaji wa viwanda na miundombinu, ikiwemo reli hadi kufikia hatua ya kufa.

Amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha wanatembelea viwanda vyote ili kufahamu vile vinavyofanyakazi na visivyofanyakazi kwa lengo la kuvirejesha na kuwapa watu, ambao wana nia ya kuwekeza.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli amewataka mawaziri wanaohusika na mchakato wa ufungaji wa mita za kupima mafuta, wajipange kuhakikisha wanaharakisha na kwamba, kuna hofu ya harufu kubwa ya rushwa ndani yake.

Amesema tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotoa agizo la kufungwa kwa mita hizo, umepita mwaka sasa na wapo baadhi ya mawaziri wamekuwa wakishindwa kutoa maamuzi kutokana na sababu za kipumbavu.

Rais Dk. Magufuli alisema kinachoonekana katika ufungaji mita hizo ni harufu kubwa ya rushwa na hivyo kusababisha kutofahamu kiasi gani cha mafuta kinachopotea na kwamba, suala hilo ni hasara kwa taifa.

"Nimejitoa kupambana na rushwa na watakaokutana na upepo wangu watakumbwa nao bila ya kuwaonea uhuruma. Inavyonyesha ni kuwa Waziri Mkuu alitoa agizo, lakini kinachofanyika ni ujanja ujanja unaofanywa na baadhi ya watendaji, hususan baadhi ya mawaziri, kushindwa kutoa maamuzi ya ufungaji mita hizo kwa kutoa sababu za kijinga," alisema.

Aliongeza kuwa  jukumu hilo la ufungaji mita hizo ni la Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na zabuni ya ufungaji imekwishatangazwa na kwamba, cha kushangaza hadi sasa halijatekelezwa kutokana na harufu hiyo ya rushwa.

No comments:

Post a Comment