Sunday, 13 August 2017

10 KUTOA USHAHIDI KESI YA MANJI



UPANDE wa Jamhuri umeieleza mahakama kuwa, unatarajia kuita mashahidi takriban 10, katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, inayomkabili mfanyabiashara Yusufali Manji.

Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis, alieleza hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, muda mfupi baada ya kumsomea mshitakiwa huyo maelezo ya awali.

Vitalis aliiomba mahakama hiyo kuipanga kesi hiyo kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo, ambazo wanatarajia watakuwa wameshafunga ushahidi kwa upande wao. Aliomba shauri hilo kupangiwa Agosti 22, 23 na 25, mwaka huu.

Mawakili wa utetezi Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Moses Kimaro hawakuwa na pingamizi kuhusu tarehe hizo.

Awali, akimsomea maelezo ya awali, ambayo Manji alikubali ni maelezo yake binafsi huku akikana mengine, Wakili Vitalis alidai mshitakiwa huyo ni mfanyabiashara na alituhumiwa kwa kujishughulisha na dawa za kulevya na kutumia.

Vitalis alidai  Februari 9, mwaka huu, mshitakiwa huyo aliripoti kituo cha polisi, ambapo alipelekwa kupekuliwa nyumbani kwake Sea View, Kivukoni na kwa Mkemia Mkuu wa serikali, alikochukuliwa haja ndogo, ambayo iligundulika kuwa na 'benzodiazepine'.

Wakili huyo alidai, mshitakiwa huyo alifunguliwa mashitaka ya matumizi ya dawa za kulevya.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Manji alikubali maelezo yake binafsi, ikiwemo majina yake na kwamba, yeye ni mfanyabiashara na mahali anapoishi huku mengine akikana. 

Shauri hilo limepangwa kuanza kusikilizwa Agosti 22, 23 na 25, mwaka huu.

Kwa mara ya kwanza, Manji alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Februari 16, mwaka huu, kujibu mashitaka ya kutumia dawa za kulevya.

Manji anadaiwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu, eneo la Upanga Sea View, wilayani Ilala, Dar es Salaam,  alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

No comments:

Post a Comment