SERIKALI imevitwaa viwanda 10 kati ya 156, vilivyoko nchini, kufuatia agizo la Rais Dk. John Magufuli, la kutwaa viwanda vilivyobinafsishwa, lakini hadi sasa vimeshindwa kufanya kazi.
Hatua hiyo ilifikiwa katika kikao cha kamati maalumu, kilichokutana mjini hapa jana na kuzijumuisha Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wataalamu, ofisi za wakuu wa mikoa na wizara za kisekta, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Msajili wa Hazina, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alitoa taarifa hiyo mjini hapa, jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya kamati hiyo kukutana.
Mwijage alivitaja viwanda vilivyochukuliwa na umiliki wake kurejeshwa serikalini kuwa ni Kiwanda cha Korosho Lindi, Mgodi wa Pugu Kaolin na Kiwanda cha Mkata Saw Mills Ltd.
Vingine ni Manawa Ginnery Co. Ltd, Dabada Tea Factory, Tembo Chipboards Ltd, Kilimanjaro Textile Mills, Mang’ula Mechanical and Machine Tool Co. Ltd, Mwanza Tenneries Ltd na Polysacks Co. Ltd.
Alisema mashirika 341, yalikuwepo katika mchakato wakati wa ubinafsishaji, lakini hivi sasa serikali imeamua kuelekeza nguvu zake kwenye viwanda.
Mwijage alisema kufuatia tathmini iliyofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina mwaka 2015/16, kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ilianisha utendaji wa viwanda hivyo, ambapo 62 ilibainika vinafanyakazi vizuri, 28 vinafanya kazi kwa kusuasua na 56 vilikuwa vimefungwa.
Akifafanua kuhusu viwanda vilivyofungwa, alisema mpaka sasa 11 vimeanza kazi na kwamba, wamiliki wake wamezingatia agizo la serikali.
Waziri Mwijage alivitaja viwanda vilivyoanza kazi kuwa ni MOPROCO, Ubungo Garments Ltd, Kilichokuwa Kiwanda cha Morogoro Shoe na Kibaha Garments Ltd. Vingine ni Kibaha Cashew Nut Plant, Shinyanga Meat Factory, Morogoro Canvas Mill (MCC), Kinu cha Manonga, Mwatex, Urafiki na Mitex.
Mwijage alisema kazi ya kutwaa viwanda visivyofanya kazi ni endelevu na mpaka hivi sasa kikosi kazi, wakiwemo wakuu wa mikoa, wapo kazini nchi nzima ili kubaini viwanda, ambavyo havifanyikazi na kuvitolea maamuzi. Alisema watafikia kikomo Agosti 22, mwaka huu.
Alisema msajili wa hazina ndiye mwenye mamlaka ya kuwapatia viwanda watu wanaohitaji kuvimiliki, vile ambavyo vimerejeshwa serikalini.
No comments:
Post a Comment