Sunday, 13 August 2017

MAREKANI, BILL GATES WAITENGEA TANZANIA MABILIONI


Taasisi ya Bill and Mellinda Gates, imetenga sh. bilioni 777.084 kwa  ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya na mifumo ya kielektroniki ya upatikanaji wa taarifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo, Bill Gates, Ikulu, Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli.

Gates, alisema taasisi yake inashirikiana na Tanzania kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini.

Alisema fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi zaidi ya afya, ikiwemo kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na ugonjwa wa malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na utapiamlo.

Pia, alisema fedha hizo zitatumika katika sekta ya kilimo, ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na pia zitasaidia kuweka mifumo ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa.

Mwenyekiti Mwenza huyo alifurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania
na pia uongozi na msimamo wa Rais Magufuli, kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa.

Alisema atakuja nchini mara nyingi ili kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alimshukuru Gates kwa mchango mkubwa unaotolewa na Taasisi ya Bill and Mellinda Gates, katika miradi mbalimbali nchini, ikiwemo fedha ambazo itazitoa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.

Rais Dk. Magufuli alimhakikishia Gates kuwa, serikali yake itahakikisha fedha hizo zinaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Gates, yalihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na uvuvi, Dk. Charles Tizeba na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Wakati huo huo, Rais Magufuli, jana, alikutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk. Inmi Patterson, ambaye alisema Marekani itatoa fedha za nyongeza Dola milioni 225, sawa na sh. bilioni 499.500 za Tanzania, katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora, utawala bora.

Patterson, amesema Marekani imeongeza fedha hizo katika miradi inayotekelezwa hapa nchini kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania na itahakikisha uhusiano na ushirikiano huu unaendelezwa na kukuzwa zaidi.

Kwa upande wake, Rais Magufuli alimshukuru Balozi Patterson kwa mchango mkubwa, ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania.

Alimhakikia kuwa serikali itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano wake na Marekani, na pia amemuomba awahimize wafanyabiashara na wawekezaji wengi zaidi wa Marekani, waje kuwekeza na kufanyabiashara hapa nchini kutokana na fursa lukuki zilizopo.

Pia, aliiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya kitaifa katika makao makuu ya nchi mkoani Dodoma, ili kuongeza uwezo wa mkoa huo kutoa huduma za matibabu, ikilinganishwa na ilivyo sasa.

No comments:

Post a Comment