Sunday 13 August 2017

TAKUKURU KUONGEZA NGUVU YA KIMATAIFA SAKATA LA TEGETA ESCROW


HALI ni tete kwa vigogo kwenye sakata la Tegeta Escrow, baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kusema kuwa imeamua kuzishirikisha taasisi nyingine za kimataifa ili kuchunguza kama wahusika wamehifadhi fedha nje ya nchi.

Tayari TAKUKURU imeeleza kwamba, inaendelea kufuatilia fedha hizo zilizopelekwa nje na watuhumiwa wote ili kuhakikisha haki inatendeka.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki, Ofisa Habari na Uhusiano wa taasisi hiyo, Mussa Misalaba, alisema watu hao wanaendelea kuchunguzwa na TAKUKURU kwa kushirikiana na baadhi ya taasisi za nje
na kwamba, uchunguzi huo unafanyika kwa umakini mkubwa.

"Hili jambo linafanyika kwa umakini mkubwa, usione kimya, kuna jambo linafanyika, ni mapema mno kusema,"alisema Misalaba.

kuhusu idadi ya wahusika wanaochunguzwa, ambao wamehifadhi fedha nje ya nchi, Misalaba hakuwa tayari kuwataja kwa madai kuwa, kazi hiyo inafanyika kwa usiri na ikikamilika, watawataja wahusika wote.

Hivi karibuni, TAKUKURU iliwafikisha mahakamani baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi na uhujumu uchumi ili  kujibu mashtaka yanayowakabili.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni wake wanaohusishwa na kashfa ya wizi wa zaidi ya shilingi bilioni 300, kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Watuhumiwa hao walifikishwa kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam, ambapo kila mmoja anakabiliwa na shitaka moja la kula rushwa.

Mshitakiwa wa kwanza kupandishwa kizimbani alikuwa Theophilo  Bwakea, ambaye inadaiwa kuwa, Februari 12, mwaka 2014, alitenda kosa hilo, baada ya kupokea kiasi cha sh. milioni 161.7, kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Kiasi hicho cha fedha kinachodaiwa kuwa ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, kilitolewa kupitia akaunti ya mshtakiwa yenye namba 00410102643901 ya benki ya Mkombozi.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa  Rugemarila, ikiwa ni sehemu ya shukrani zake kwa baadhi ya wajumbe waliohusika kuandaa sera ya sekta binafsi ili watengeneze mazingira mazuri sekta hiyo kuzalisha na kuiuzia umeme TANESCO.

Mshitakiwa wa pili kupandishwa kizimbani alikuwa Rugonzibwa Mujunangoma, ambaye anadaiwa Februari 5, mwaka 2014, kwenye jengo la Benki ya Mkombozi, Ilala, Dar es Salaam, alipokea rushwa ya sh. milioni 323.4, kutoka kwa Rugemarila.

Rugonzibwa, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Kisheria katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anadaiwa alipokea kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake yenye namba 00120102602001, kinachodaiwa kuwa ni sehemu ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

Pia, fedha hizo zinadaiwa kuwa ni shukrani kwa Rugemarila kwa mkurugenzi huyo, kutokana na mchango wake wa kuiwezesha IPTL Tanzania Ltd, kuwa mfilisi wa muda.

Hata hivyo, watuhumiwa wote walikana mashitaka yaliyosomwa mbele yao na Ofisa wa TAKUKURU, Benard Swai.

Sakata hilo pia lilisababisha baadhi ya viongozi kujiuzulu, akiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema huku Rais mstaafu Jakaya Kikwete akitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa  Anna Tibaijuka wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisimamishwa  kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake kutokana na kuhusishwa na kashfa hiyo.

Pia, TAKUKURU imewafikisha mahakamani, mmiliki wa Kampuni ya PAP, Habirnder Seth Singh na mfanyabiashara Rugemalira, kwa makosa ya uhujumu uchumi na kesi hiyo bado inaendelea kusikilizwa.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, aliwahi kusema kuwa, watawafikisha mahakamani watuhumiwa wote kwa makosa ya kuhujumu uchumi na mengine yanayofanana na hayo.

Mlolowa alisema ukimya wa taasisi yake ulikuwa kwa sababu ya uchunguzi uliokuwa unaendelea kwa muda mrefu na kwamba, ukikamilika watafikishwa mahakamani baada ya hatua za awali za uchunguzi kukamilika.

No comments:

Post a Comment