Sunday 13 August 2017

UHAMIAJI SASA WATINGA NYUMBA ZA IBADA



TAASISI za dini nchini zilizoajiri wageni, zimetakiwa kufuata sheria ya Uhamiaji, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kuwakamata raia wa kigeni.

Idara ya Uhamiaji imeamua kuzigeukia taasisi hizo na kuzitaka kufuata sheria ya vibali vya kazi na ukaazi vinavyotolewa kwa mujibu wa taratibu, ambavyo vinatolewa bila ya misingi ya ubaguzi wa dini au dhehebu.

Pia, imezitaka taasisi  za dini zenye sifa za kupewa misamaha ya vibali vya kazi, kuwasilisha maombi yao Wizara ya Kazi na Ajira na baadaye Uhamiaji.

Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano na Msemaji Mkuu wa Idara hiyo, Mrakibu Ally Mtanda, alipowasilisha mada juu ya Uraia na Uhamiaji, katika semina iliyoandaliwa na Kanisa la The Pool of Silom Church, lililoko Mbezi Beach, Makonde, nje ya jiji la Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.

Washiriki 650 kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, walishiriki katika semina hiyo, iliyoanza Agosti Mosi na inatarajiwa kufungwa Jumapili ijayo na kisha kuhamia mikoani, ikianza na Mbeya.

Alisisitiza kuwa kamwe serikali kupitia Idara ya Uhamiaji, haitatoa vibali vya ukaazi kwa misingi ya ubaguzi wa rangi, kabila, dini au itikadi za vyama bali itafuata sheria zilizopo.

Mtanda alisema Idara ya Uhamiaji  imejipanga kuhahakisha huduma zake zinawafikia wananchi popote walipo bila ya ubaguzi.

Alisema lengo ni kuwajengea uelewa viongozi wa dini  kuhusu mambo yanayofanywa na Uhamiaji, kwa kuwa wanatambua kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni shirikishi na  wananchi,  hasa viongozi wa dini wana mchango mkubwa.

"Ukweli viongozi wa kidini ni kioo mbele ya jamii, napenda kuwapongeza na jambo la msingi hapa ni kuwataka kuzingatia sheria za uhamiaji ili tujenge nchi yetu na kuendelea kuwa kisiwa cha amani,"alisema.

Aliwashukuru viongozi wa taasisi hiyo, hasa baba wa kiroho 'MPAKA MAFUTA' kwa kutambua umuhimu wa kuandaa semina hiyo na kumpa mwaliko kwa niaba ya Idara ya Uhamiaji.

Akizungumzia kuhusu mada ya Uraia na Uhamiaji, alisema  dhana ya uraia na nani ni raia wa Tanzania, ni suala muhimu na ndiyo msingi wa taifa lolote lile duniani.

Alisisitiza kuwa  taifa lolote, liwe kubwa au dogo, haliwezi kukamilika bila ya kuwa na raia wake, ndiyo maana raia wa nchi husika hutambuliwa kulingana na mataifa yao, mfano Tanzania (Watanzania), Kenya (Wakenya), Uganda (Waganda) na Malawi (Wamalawi).

No comments:

Post a Comment