Saturday, 5 March 2016

MAJALIWA ATOA SIKU 13 KWA DC BARIADI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku 13 kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Ponsiano Nyami na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Mathias Mkumbo, wahakikishe wanafunzi 583, waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, wawe wameripoti kwenye shule walizopangiwa.

Majaliwa, ameagiza kutafutwa kwa wanafunzi hao popote walipo na wapelekwe shuleni ili waungane na wenzao na kuwachukulia hatua wazazi, ambao watoto wao wamefaulu, lakini wanachunga ng’ombe.

Alisema serikali imeamua kuanzisha sera ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne na kuwapunguzia wazazi na walezi mzigo wa ada na michango ili kutoa fursa kwa watoto wote waliochaguliwa kuweza kuendelea na masomo.

Majaliwa aliyasema hayo juzi, alipozungumza na wananchi wa wilaya ya Bariadi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM.

Aliwataka viongozi wa wilaya kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti katika shule walizopangiwa na ifikapo Machi 15, mwaka huu, awe amepelekewa taarifa.

“Natakata watoto wote hawa 583 ambao hawajaripoti shuleni watafutwe popote walipo na ifikapo Machi 15, wawe wameenda shule.

"Mkuu wa wilaya na mkurugenzi mnipatie taarifa yao na hata kama wazazi wamewatorosha, wakamatwe ili wachukuliwe hatua kwani ni lazima watoto wapate elimu na serikali haitalifumbia macho suala hili,”alisema.

Majaliwa pia aliagiza kuchukuliwa hatua kwa watu wote watakaowakatisha masomo wanafunzi, hasa wa kike na kuwataka wahusika wawalinde watoto huku wakienzi kaulimbiu ya Mke wa Rais mstaafu, Mama Salma Kikwete, isemayo ‘ mtoto wa mwenzio ni wako, mlinde’.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Nyami katika taarifa yake aliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu, alisema wanafunzi 4,474, walitarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza, ambapo hadi kufikia Februari 26, mwaka huu, wanafunzi 3,891 ndio walioripoti katika shule walizopangiwa.

Nyami alisema tayari wamewaagiza watendaji wa kata kuwaandikia barua na kuwapeleka mahakamani ifikapo Machi 15, mwaka huu, wazazi na walezi wa wanafunzi, ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, lakini hawajaripoti.

Katika hatua nyingine , Nyami alisema wilaya  hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati, ambapo kwa sasa yapo 19,900 kati ya 45,471, hivyo kuwa na upungufu  madawati 25,571.

No comments:

Post a Comment