Saturday, 5 March 2016
RC CHIKU: WAKURUGENZI WA HALMASHAURI NI MAJIPU
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa, amesema wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo ni jipu linalotakiwa kukamuliwa, kutokana na kushindwa kuwasimamia wananchi kuzuia ugonjwa wa kipindupindu.
Chiku, alisema hayo jana, wakati akizungumza na watendaji wa afya, kuhusu hali ya kipindupindu mkoani hapa.
Alisema licha ya serikali ya mkoa huo kuunda timu mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo kwenye wilaya, bado unaendelea kutokana na kukosekana kwa ufuatiliaji.
Chiku alisema timu hizo zilikuwa na kazi ya kupita na kuangalia hali ya usafi katika kila kaya na kutoa taarifa kwa wakurugenzi kila siku asubuhi.
Alisema pamoja na kuweka utaratibu huo, hakuna mkurugenzi ambaye amefuatilia na kwamba ugonjwa huo umeendelea kuenea kwa kasi.
“Hivi sasa hata nikisema mkurugenzi mmoja anionyeshe taarifa ya kamati yake hakuna, na nyinyi ni majipu yanahitaji kukamuliwa, nataka ifikapo Machi 15, mwaka huu, nisisikie kipindupindu mkoani hapa,’’ alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kwa sasa wilaya ya Kondoa ndio inayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi, ambapo hadi jana walikuwa 21.
Akizungumza katika kikao hicho cha watendaji wa afya, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Chatora Rufalo, alisema ugonjwa huo bado ni tishio, si kwa Tanzania pekee, bali nchi nyingi za kiafrika.
Rufalo alisema kikubwa kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya athari za ugonjwa huo na dalili zake.
Alisema hakuna sababu ya kusukumana katika kuwataka wananchi kuwa wasafi, bali elimu ni jambo la msingi kwa sasa.
Kwa mujibu wa Rufalo, shirika hilo litashirikiana bega kwa bega na Tanzania katika kutokomeza ugonjwa huo kwa kutoa kila msaada unaotakiwa, ikiwa ni pamoja na dawa za kutibu maji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment