POLISI mkoani Arusha, imekamata bunduki nne za kivita na nyingine 30 za kiraia zilizosalimishwa katika vijiji vya Kisangiro na Naane wilayani Ngorongoro.
Silaha hizo zilikamatwa wiki hii, baada ya kutelekezwa na watuhumiwa, walipokuwa wakiwakimbia polisi waliotaka kuwatia nguvuni.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa, silaha nyingine zilikamatwa kutokana na agizo la kuwataka wanaozimiliki isivyo halali na wanaozimiliki kisheria, kuzisalimisha kwa mkuu wa polisi Ngorongoro.
Alizitaja bunduki hizo za kivita kuwa ni G.3, moja ikiwa haina risasi, SMG mbili, moja ikiwa na risasi saba na nyingine risasi tatu na AK 47 ikiwa na risasi tatu.
Sabas alisema silaha za kiraia zilizosalimishwa ni 30, zikiwemo bunduki aina ya Rifle 19, bastola mbili, shortgun tisa na risasi 194.
“Tumebaini silaha nyingi zinamilikiwa kihalali, lakini zinatumika katika vitendo vya uhalifu, ikiwemo ujangili na ujambazi,” alisema Sabas.
Alisema sehemu kubwa ya silaha hizo zinamilikiwa na wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60, ambapo vijana wao hutumia fursa hiyo kuzitumia kwenye uhalifu.
Kamanda Sabas alitoa onyo kwa wananchi kwa kusema kuwa, kazi ya kusaka silaha inaendelea na watakaokaidi kuzisalimisha au watakaokamatwa wakizimiliki kinyume cha sheria, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Kufanyika kwa operesheni hiyo kunatokana na mauaji ya watu watatu yaliyotokea Februari 12, mwaka huu, saa tatu usiku, katika kitongoji cha Meje, kilichoko kijiji cha Kisangiro.
Katika tukio hilo, watu hao waliuawa kwa kupigwa risasi wakiwa wamejipumzisha karibu na boma la Elias Mesoi, ambaye ni mkulima.
No comments:
Post a Comment