Saturday, 5 March 2016

MLIPUKO WA BOMU MASKANI YA CCM WAZUA KIZAAZAA

KIKOSI  Maalumu cha Uchunguzi wa Milipuko cha Jeshi la Polisi, kinaendelea kufanya uchunguzi wa kina kufuatia mlipuko wa bomu uliotokea kwenye kontena na maskani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), yaliyoko mtaa wa Michenzani, mjini Unguja.

Mlipuko huo ulitokea saa sita usiku wa kuamkia jana na uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa ni bomu lililotengenezwa kienyeji.
 Akizungumza na Uhuru jana, mmoja wa watu walioshuhudia mlipuko huo, Shaban Saidi, alisema aliona kikundi cha vijana wasiopungua sita, waliovaa kanzu na vitambaa vyeupe kichwani, wakiwa ndani ya gari ndogo aina ya Keri, wakilizunguka kontena hilo.

Shaban alisema dakika mbili baadaye, aliiona gari hilo likiondoka kwa mwendo wa kasi kabla ya kusikika kwa mlipuko mkubwa pembezoni mwa kontena hilo, uliosababisha baadhi ya vioo vya madirisha ya nyumba za Michenzani kupasuka.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alifika eneo la tukio na kujionea hali halisi.

Katibu wa Maskani ya CCM ya Kisonge, Mzee Yunus alimwambia Balozi Idd kuwa, vipo baadhi ya vifaa vilivyoathirika kutokana na mlipuko huo kwenye kontena hilo, ambalo linatumika kama  stoo kwa ajili ya kuhifadhi vitu vyao.

Yunus aliiomba serikali kuimarisha zaidi ulinzi katika maeneo ya umma ili kusaidia kupunguza matukio ya hujuma yanayofanywa na baadhi ya watu ambao wana chuki za kisiasa.

Balozi idd alitoa pole kwa viongozi na wanachama wa CCM na kusema uchochezi huo haufai wakati huu, ambao wanatarajia kurudia uchaguzi mkuu.

Alieleza kusikitishwa kwake na vitendo hivyo vya kihuni vinavyofanywa na baadhi watu katika baadhi ya maeneo nchini, ambavyo alisema havitoi sura nzuri mbele ya uso wa dunia.

Aliviagiza vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo ili kuwabaini wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya  sheria.

No comments:

Post a Comment