Saturday, 5 March 2016
MAJALIWA: WAZAZI WATAKAOWAOZESHA WANAFUNZI KUFUNGWA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wazazi na walezi wilayani hapa, kuacha kuwakatisha elimu ya msingi watoto wa kike kwa ajili ya kujipatia ng'ombe.
Amesema wazazi watakaoendelea kufanya hivyo, watatumikia kifungo kitakachoambatana na kazi ngumu.
Pia, amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Georgina Bundala, kuwasimamia ipasavyo watendaji wa vijiji na kata ili kumaliza tatizo la watoto wa kike kuanzia shule za msingi, ambao wanakatishwa masomo.
Amewaagiza watendaji wa kata na vijiji, kusimamia elimu kwa watoto wa kike katika maeneo yao na kuwachukulia hatua wazazi watakaowakatisha masomo, kutokana na tamaa ya kupata ng'ombe na kwamba, atakayeshindwa atafukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Majaliwa aliyasema hayo jana, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu, alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika kijiji cha Budalabujiga.
Awali, Majaliwa alizindua ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara katika Shule ya Sekondari ya Budalabujiga, ambavyo vitagharimu sh. milioni 223.33.
“Yaani we unaona ng'ombe ni muhimu kuliko elimu ya mtoto, kuanzia sasa marufuku kukatiza elimu ya mtoto wa kike, atakayebainika kushiriki katika mchakato huo, kuanzia muoaji, wazazi wake pamoja wasindikizaji, wote kila mmoja atatumikia kifungo jela kitakachoambatana na kazi ngumu,”alisema.
Aliwataka watendaji wa kata na vijiji kuwa makini kwa sababu iwapo mtoto atayepata ujauzito na kukatishwa masomo yake bila ya kuwachukulia hatua wahusika, watafukuzwa kazi na kisha watafikishwa mahakamani kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Wakati huohuo, Majaliwa amewataka watoto kuwa makini na kutokubali kudanganyika na mafataki na iwapo watasumbuliwa, wawakatalie na wawaeleze kuwa wao bado wanasoma wasiwasumbue.
Akizungumzia suala la maabara, Majaliwa alisema serikali itapeleka vifaa vya maabara ili wanafunzi waweze kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo, jambo litakalowaongezea uelewa na kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa ya kumaliza kidato cha nne.
Pia, aliwataka wananchi washirikiane na viongozi, akiwemo mbunge wa jimbo hilo, Njalu Silanga, katika kuboresha maendeleo na wasikubali watu wachache wasiotaka maendeleo wawashawishi kutoshiriki shughuli za maendeleo au kubishania mambo yasiyokuwa na tija.
“Kauli ya Rais Dk. John Magufuli ya 'Hapa Kazi Tu' hakuileta kwa ajili ya kuimba na kuwafurahisha, bali amelenga kuhamasisha watu kufanya kazi, hivyo lazima kila mmoja afanye kazi ili waweze kupata maendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, John Lyimo, akizungumzia kuhusu ujenzi wa maabara, alisema lengo ni kutekeleza agizo la serikali la kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na vyumba vitatu vya maabara ili wanafunzi waweze kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo.
Alisema hadi kukamilika kwa jengo hilo, litagharimu sh. milioni 223.33, ambapo kwa sasa tayari limegharimu sh. milioni 180.95.
Kati ya fedha hizo, sh.milioni 136.83 ni nguvu kazi na michango ya wananchi wakati Halmashauri ya Wilaya imetoa sh. milioni 38.40 na wadau wa maendeleo ya elimu wametoa sh. milioni 5.72.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment