KASI ya utendaji ya Rais Dk. John Magufuli,
imeendelea kuwakuna Watanzania ambapo, uongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, umeeleza
kuvutiwa na kupongeza utendaji kazi wake.
Pia, umesema uamuzi wa Dk. Magufuli kuanza
kudhibiti matumizi ya fedha za serikali kwa kuzuia safari za nje ya nchi kwa
viongozi na watendaji wa wizara na taasisi, ni hatua ya kuungwa mkono.
Chama hichi kimesema uamuzi huo unadhihirisha
dhamira ya kweli ya Dk. Magufuli kuwatumikia Watanzania na kuwabana watendaji
kutimiza majukumu yao.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alifuta safari za nje
ya nchi kwa viongozi wa umma na kuagiza shughuli hizo ziwe zinafanywa na
mabalozi.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema vibali vyote vya
safari hizo vitakuwa vinatolewa na yeye mwenyewe pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Ombeni Sefue.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiongozi
Mkuu wa ACT, Zitto Kabwe alisema anampongeza Dk. Magufuli kwa kudhibiti safari
hizo.
Zitto alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC), kamati yake iliagiza ufanyike ukaguzi maalumu wa
safari za nje kwa viongozi na tayari ripoti imekamilika.
Zitto alimpongeza Mwenyekiti wa taifa wa chama
hicho, Anna Mghwira, kwa kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi mkuu wa rais, ambapo
katika wagombea wanane, mwanamke alikuwa peke yake.
Pia, aliwashukuru wananchi kwa kukiwezesha chama
hicho kushika nafasi ya tatu katika kinyang’anyiro cha kumpata rais licha ya
uchanga wake na kuviacha nyuma vyama vikongwe.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo,
Samson Mwigamba amesema chama hicho hakitakuwa na mgombea wa uspika, badala
yake wanajikita katika uchaguzi mdogo wa majimbo manane.
Mwigamba alisema hawatajihusisha katika mchakato
wa kusimamisha mgombea wa uspika kwa sababu wamewekeza nguvu zaidi katika
uchaguzi mdogo wa wabunge, ambao utafanyika katika majimbo manane, ambayo
hayakupika kura Oktoba 25, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment