WAGOMBEA kumi wamechukua fomu ya kugombea kuteuliwa
kwa nafasi ya uspika na unaibu
spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Miongoni mwa waliochukua fomu ni Leonce
Mulenda,Profesa Costa Ricky Mahalu, Samwel Sitta, Dk. Kalokola Muzzammil, George
Nangale, Banda Sonoko,Gosbert Blandes, Simon Rubugu, Balozi Philip Marmo na
Dk.Emmanuel Nchimbi.
Fomu hizo zilianza kutolewa jana, kwenye Ofisi Ndogo
ya Makao Makuu ya Lumumba, jijini Dar es Saalam na Katibu wa Organezesheni, Dk.Muhammed
Seif Khatib, kuanzia saa sita mchana.
Dk.Khatib alisema kwa wagombea ambao sio wabunge,
mwisho wa kurejesha fomu hizo ni leo saa kumi jioni na kwa wale, ambao ni
wabunge wateule, mwisho wa kuzirejesha ni keshokutwa.
“Baada ya kurejesha fomu, majina yao yatapelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuthibitisha
kama wana sifa za kugombea nafasi hiyo,”alisema
Alisema hatua itakayofuata ni kuwajadili na kuwachuja
kupitia Kamati Kuu ya CCM na Kamati ya Chama ndani ya bunge, ili kumchagua
mmoja wao na kwamba vitu vitakavyozingatiwa ni masharti.
Alisema jumla ya wajumbe 246 watashiriki katika kupitisha
jina hilo la mgombea.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua
fomu, spika wa zamani wa bunge, Samuel Sitta, alisema lengo kuu la kujitosa
kwenye kinyanganyiro hicho ni kutokana na kuwa na sifa za kutosha na uzoefu
mkubwa.
Alisema anataka kuendeleza mipango ya kimaendeleo ya
bunge, ikiwemo kurejesha nguvu ya chombo hicho na hadhi yake.
“Katika bunge la tisa niliweka mipango hiyo, lakini
kwa bahati mbaya ikashindwa kuendelezwa, lakini kwa sasa nina imani kuwa bunge
hili litakuwa gumu kutokana na changamoto za kuwepo kwa suala la katiba, mambo
ya siasa za ukanda na masuala ya kipato,”alisema
Kwa upande wake, Dk. Nchimbi alisema dhamira ya
kujitokeza kuchukua fimu hiyo ni kutokana na changamoto za wakati huu, ambapo
wabunge hawashiriki kikamilifu katika kuwaletea maendeleoa wananchi ipasavyo.
Dk.Nchimbi alisema kasi ya Rais Dk. John Magufuli
inatakiwa kuendana sawa na viongozi wengine ili kutekeleza Ilani na ahadi za
CCM, ambazo ni kuwaletea maendeleo Watanzania bila kujali itikadi za vyama.
“Ninachosema ni kwamba nimejitokeza kutokana na
kujipima kuwa uwezo wangu ni mzuri, pia nina sifa za kushika nafasi hiyo kwa
kasi kama ya Rais Magufuli ili kuwaletea maendeleo wananchi,”alisema
Wakati
huo huo, CCM imetoa ratiba ya kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa uspika na
unaibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo wana-CCM wasio
wabunge wenye sifa walitakiwa kuchukua fomu jana.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, ilisema
fomu hizo zitatolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Oganaizesheni,
Muhammed Seif Khatib na zilianza kutolewa jana, saa 6.00 mchana na mwisho wa
kuzirejesha ni leo kabla ya saa 10 jioni.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, fomu zitatolewa kwa wana-CCM wenye sifa husika.
Katika
taarifa hiyo, wana-CCM wasio wabunge wanaoomba ridhaa ya Chama kugombea uspika,
wanatakiwa kuchukua fomu hizo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba
jijini Dar es Salaam na kuzirejesha leo, kabla ya saa kumi jioni.
Aidha,
taarifa hiyo ilisema wana-CCM, ambao ni wabunge wateule wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, wanaoomba kuteuliwa kugombea uspika na unaibu spika wa
bunge, walitakiwa kuchukua fomu kuanzia jana na kuzirejesha Novemba 14, mwaka
huu, kabla ya saa kumi jioni, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM,
Lumumba, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment