HATIMAYE Hospitali ya Taifa Muhimbili imelazimika
kutumia saa mbili kukarabati mashine ya kuchunguzia magonjwa ya MRI, baada ya Rais
Dk. John Magufuli, kutoa siku 14 kwa uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha mashine
hiyo na ya CT-SCAN zinakarabatiwa.
Rais Magufuli, hivi karibuni alifanya ziara ya
kushitukiza kwenye hospitali hiyo na kuwataka watumishi wake kufanyakazi na
kuonya kuwa hatamuonea huruma yeyote atakayeshindwa kuwahudumia wananchi.
Mashine hiyo ilianza kufanyakazi jana alasiri, baada ya
mafundi kutoka Kampuni ya Philips, kufanya matengenezo kuanzia mchana.
Aidha, mafundi hao wanaendelea kuifanyia matengenezo
mashine ya CT- SCAN, ambayo nayo wakati wowote inatarajiwa kutengemaa na kuanza
kutoa huduma kwa wagonjwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, ilisema
leo watatoa taarifa kuhusu hatua za ukarabati za mashine hiyo zilipofikia.
Kurejea kwa huduma za vipimo vya MRI katika hospitali
hiyo ya taifa, kutawawezesha wagonjwa kufanyiwa vipimo vya picha kwa ubora bila
kutumia mionzi.
Ziara ya Rais Magufuli, imekuwa mkombozi kwa wagonjwa
hususan waliokuwa wakihitaji huduma za vipimo hivyo, iliyokosekana kwa zaidi ya
miezi miwili.
Baada ya ziara hiyo aliyoifanya Novemba 9, mwaka huu,Rais
Magufuli alivunja bodi ya hospitali hiyo, ambayo ilishamaliza muda wake, na
kumrudisha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Kidanto, aliyekuwa
anakaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu.
Rais huyo wa awamu ya tano, alionyesha kukerwa na
vitendo vinavyofanywa kwa makusudi na baadhi ya madaktari, kuharibu vifaa tiba
kisha kuwaelekeza wagonjwa kufuata huduma hizo kwenye hospitali binafsi.
No comments:
Post a Comment