Wednesday, 8 June 2016
WANAOINGILIA BARABARA ZA DART KUSHUGHULIKIWA
SERIKALI imesema itawachukulia hatua za kisheria watumiaji wa barabara wanaoingilia njia maalumu zilizotengenezwa kwa ajili ya Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (DART).
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Mollel.
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali wa kupunguza ajali za barabarani, hususan za mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam, kutokana na kuwepo kwa madereva wazembe.
Kwa mujibu wa Amina, hadi sasa mabasi 30 ya DART yameshapata ajali na kuigharimu serikali sh.milioni 90 kwa ajili ya matengenezo.
Akijibu swali hilo, Simbachawene alisema madereva mbalimbali wakiwemo wa pikipiki, bajaji na magari mengine bado wameendelea kutumia barabara hizo.
Alisema utumiaji wa barabara hizo ni kuvunja cha sheria kwa kuwa zimejengwa kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka, lengo likiwa ni kupunguza foleni katika jiji hilo.
“Barabara hizi zilijengwa kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka,
hivyo kwa madereva wengine wanaoendelea kutumia barabara hizo, wanavunja sheria na ajali inapotokea, dereva wa aina nyingine ya usafiri tofauti na mabasi yaendayo kasi, ndiye anakuwa na kosa la kuligonga basi hilo,”alisema Simbachawene.
Aliwataka madereva kutoendelea kutumia barabara hizo na kuziheshimu ili kuokoa fedha za serikali kwa ajili ya kufanya matengenezo pindi mabasi hayo yanapogongwa.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salim, aliitaka serikali kutoa idadi ya ajali zilizotokea barabarani, baharini na kwenye maziwa katika kipndi cha Januari, 2015 hadi sasa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, alisema katika kipindi cha Januari, 2015 hadi Februari, 2016, jumla ya ajali za barabarani zilikuwa 9,864, zilitokea na kusababisha vifo 3,936 na majeruhi 9,868, katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment