Wednesday, 8 June 2016
ALIYEMTUSI JPM ATOZWA FAINI SHILINGI MILIONI SABA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imemhukumu kulipa fani ya sh. 7,000,000, Isack Habakuki (40), mkazi wa Olasiti, mjini Arusha, aliyepatikana na hatia ya kumtukana na kumdhalilisha Rais Dk. John Magufuli, kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Arusha, Agustino Rwizile, baada ya mshitakiwa kukiri kutenda kosa hilo mbele ya mahakama, baada ya kusomewa maelezo ya awali.
Kwa mujibu wa Hakimu Rwizile, adhabu ya kosa hilo chini ya sheria mpya ya makosa ya mitandao ya mwaka 2015, ni kifungo cha miaka mitatu jela, faini ya sh. 5,000,000 au vyote kwa pamoja.
Baada ya hukumu hiyo, Wakili wa utetezi, Wakili Mosses Mahuna, aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu mteja wake kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kutenda kosa hilo na kwamba, anayo familia, wakiwemo wazazi, ambao wanamtegemea, hivyo kuiomba imhukumu kulipa faini badala ya kifungo.
“Mheshimiwa hakimu, kupitia kifungu namba 330 (3) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (20), kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mahakama inampa mtuhumiwa haki ya kuhumiwa kifungo gerezani au kulipa faini, hivyo naomba mteja wangu alipe faini badala ya kutumikia kifungo,” alidai wakili huyo wa utetezi.
Akijibu hoja ya wakili huyo, Hakimu Rwizile alisema kosa alilotenda mtuhumiwa si dogo kwa kuwa aliyemtukana na kumdhalilisha ni rais aliyechaguliwa na mamilioni ya wananchi kwa kupigiwa kura.
“Sheria ya makosa ya mitandao zimetungwa ili kila mmoja aweze kutumia simu yake pamoja na mitandao ya kijamii bila kuvunja sheria za nchi, kwani hata mtoto mdogo hapaswi kutukanwa na kudhalilishwa kiasi hicho,”alisema.
“Kwa kuwa umemdhalilisha rais aliyechaguliwa na watu, utalipa faini ya sh.milioni saba kwa awamu mbili, awamu ya kwanza sh.milioni tatu na ya pili Julai 7, mwaka huu na kiasi kilichosalia utakilipa Agosti 8, mwaka huu. Ukishindwa kufanya hivyo, utakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitatu,”alisema
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Timonth Vitalis, alidai mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 17, mwaka huu kwa kumtukana na kumdhalilisha Rais Magufuli, kwamba siasa anazofanya ni za maigizo na kumfananisha na bwege.
Wakili Vitalis alidai mtuhumiwa huyo alituma ujumbe kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa facebook na kuwataka watu kutoa maoni kuhusiana na Rais Magufuli, ambapo aliandika: "Hizi siasa ni za maigizo, halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere, wapi bwana."
Baada ya kusoma maelezo ya kosa, wakili huyo wa serikali aliwasilisha mbele ya mahakama vielelezo vinane, ikiwemo simu ya mkononi ya mtuhumiwa huyo aina ya Tecno, iliyokuwa na kadi ya simu ya mtandao wa Vodacom na Airtel, ambayo imetaifishwa na mahakama hiyo baada ya hukumu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment