Wednesday, 22 March 2017

MWENYEKITI, MAKAMU WAKE WAJIUZULU KAMATI YA BUNGE


MWENYEKITI na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, wamejiuzulu nafasi zao kwa madai kuwa wanahitaji muda mwingi wa kuwahudumia wapigakura wao.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti, Dk. Balali Kafumu na makamu wake, Vicky Kamata, walisema wamejiuzulu nafasi hizo kwa hiari yao.

Dk. Kafumu alisema akiwa mwenyekiti wa kamati hiyo, ameshindwa kuhudhuria vikao mbalimbali jimboni kwake, ikiwa ni pamoja na vikao vya mabaraza ya madiwani.

Alisema uenyekiti wa kamati hiyo umemchukulia muda mwingi wa kuwahudumia wananchi wake.

“Kazi ya uenyekiti ni kazi ngumu na inachukua muda mrefu, sasa naona nikiendelea kuifanya, nitakosa nafasi ya kuwahudumia wananchi, hivyo nikaona nilete barua ya kujiuzulu nafasi hii.

"Nawashukuru wananchi na serikali kwa kutaka kuipeleka nchi hii katika nchi ya viwanda, najua kazi hiyo ni kubwa na ni moja ya kamati iliyopewa kazi kubwa kwani mpango wa miaka mitano wa maendeleo umesimamia katika kuipeleka nchi katika ngazi ya viwanda,’’ alisema.

Mwenyekiti huyo aliyejiuzulu alisema, endapo angeendelea na nafasi hiyo, angekosa nafasi ya kufanya mambo mengine, hivyo ameamua kujiuzulu.

“Wakati mwingine kama kamati tumekuwa tukifanya kazi usiku na mchana, hivyo tumekuwa tukikosa nafasi ya kufanyakazi ya wananchi,’’alisema.

Kafumu alisema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, kamati hiyo ilikumbana na changamoto mbalimbali na wakati mwingine iliweza hata kusigana na serikali, lakini lengi lilikuwa ni kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Vicky alisema ameamua kufikia uamuzi huo ili kupata nafasi ya kutosha ya kuwahudumia wanawake wa mkoa wa Geita.

“Kwa ridhaa yangu mwenyewe, nimeamua kujiuzulu nafasi hiyo ili kupata nafasi zaidi ya kuwahudumia wanawake walionichagua na kukaa na familia yangu,’’ alisema.

Alisema katika muda wa uongozi wake, anaishukuru serikali kwa ushirikiano wake kwa kamati, hasa katika kuhakikisha kuwa nchi inaenda katika uchumi wa viwanda.

Vicky alisema yeye na mwenzake kama wabunge, kazi yao ni kuisimamia serikali katika utekelezaji wa masuala mbalimbali kwa wananchi wake.

No comments:

Post a Comment