Wednesday, 22 March 2017
MAGUFULI: MAKOCHA CHAPA KAZI
RAIS Dk. John Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kufanyakazi na kuachana na maneno ya kwenye mitandao.
Aidha, amewataka Watanzania wa vyama vyote nchini, kutojisumbua na mambo yasiyokuwa na msingi kwenye mitandao kwa sababu yanapoteza muda wao mwingi.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizindua na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara za juu, katika makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Rais Dk. Magufuli alisema yeye ndiye anayeamua nani akae wapi na yupi akae wapi na hakuna wa kumpangia kwa sababu anajiamini.
"Hata siku ya kwenda kuchukua fomu, nilikwenda kuchukua mwenyewe, hakuna mtu aliyenishauri, niliamua mimi mwenyewe kwamba nafiti kuwa rais. Kwa hiyo nitaamua mwenyewe nani anatakiwa kuwa wapi, akae wapi, mimi ndiye ninayepanga,"alisema.
Kutokana na kauli hiyo, alimtaka Makonda kuchapa kazi bila kusikiliza maneno ya watu. "Nasema Makonda chapa kazi, kama wanakuandika kwenye mitandao sio shida kwangu, hata mimi wananiandika kweye mitandao kwa hiyo nijiuzulu urais? Nasema chapa kazi, hapa kazi tu," alisisitiza.
Aliongeza: "Mnahangaika, mnaposti kwenye vinini sijui, mara hivi mara vile, mpaka hata wengine mnaingilia uhuru wangu wa kuniambia nifanye hivi. Mimi huyu uniingilie? Ukiniingilia ndio umepoteza kabisa. Mimi huwa sipangiwi mambo, mimi ni Rais ninayejiamini, siwezi nikapangiwa na mtu, ninapanga mimi."
Rais Dk. Magufuli alisema pia kuwa, yeye huwa haonyeshwi njia ya kupita kwa sababu alishaonyeshwa na CCM kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Aliwataka Watanzania na wananchi wa Dar es Salaam, kuelekeza nguvu zao katika maendeleo na ustawi wa nchi.
"Niwaombe wana Dar es Salaam, ninafahamu mna uhuru wa kuzungumza kila kitu, lakini tuelekeze nguvu zetu katika maendeleo na ustawi wa nchi yetu," alisema.
"Tunajielekeza sana katika masuala ya udaku, yanayotupotezea muda, ambayo hayatupunguzii hata njaa tuliyonayo, hayatoi hata matatizo ya msongamano katika jiji la Dar es Salaam, hayatuongezei hata shibe, hayatusaidii hata kusafiri kwenda mjini, hayatusaidii hata kununua nguo, hayatusaidii hata kununua mchicha, hayatusaidii hata kupeleka watoto wetu shuleni, hayatusaidii hata kupata dawa za hospitali,"alisisitiza.
Aliwataka wananchi kuelekeza nguvu zao katika maendeleo kwa sababu hayana chama.
"Mimi nawaomba Watanzania wenzangu wa vyama vyote, ebu tujikite katika maendeleo tunachelewa mno. Tunachelewa kwa mambo yasiyo na msingi, yanatupotezea muda," alisema.
Hivi karibuni, kulizuka mijadala kwenye mitandano ya kijamii, huku baadhi ya wanasiasa wakitaka Rais Dk. Magufuli amwajibishe Makonda kwenye nafasi hiyo kutokana na kukabiliwa na tuhuma mbalimbali.
AWAONYA WATAKAOKULA FEDHA ZA MIRADI
Wakati huo huo, Rais Dk. John Magufuli amezindua na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara za juu (Flyover) kwenye makutano ya Ubungo, Dar es Salaam na kuonya kuwa, yeyote atakayepoteza fedha za mradi huo, atatumbuliwa.
Aidha, serikali imeingia mkataba na Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu nchini, ukiwemo wa barabara za juu.
Miradi hiyo ni ujenzi wa miundombinu ya usafiri katika jiji la Dar e Salaam, yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 425 na mradi wa usambazaji wa maji safi na majitaka na utunzaji wa mazingira wenye thamani ya Dola milioni 225.
Mwingine ni mradi wa kuboresha huduma katika miji ya Arusha, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Mtwara wenye thamani ya Dola milioni 130.
Kutokana na miradi hiyo, serikali itapata mkopo wa Dola bilioni 780 (sawa na sh. trilioni 1.74).
Mkataba huo wa miradi mitatu, ulitiwa saini na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mipango na Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bella Bird.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi, Rais Dk. Magufuli alisema katika mradi huo, hakuna fedha itakayopotea na iwapo kuna mtu atapoteza, atatumbuliwa.
Aidha, aliwataka wasimamizi wa mradi huo kusimamia ili uweze kukamilika kwa wakati kabla ya miezi 30, kama ilivyopangwa.
"Sioni sababu ya mradi huu kumalizika miezi 30, wakati kuna usiku na mchana na hakuna sheria inayokataza watu wasifanye kazi mchana na usiku. Fanyeni ili huu mradi ukamilike ndani ya miezi 20. Tutafurahi sana," alisema.
Alisema mradi huo wa barabara ukikamilika, utapunguza kero ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, alisema wanatarajia kujenga barabara za juu katika makutano ya Mwenge, Morocco, Magomeni na Tabata.
Rais Dk. Magufuli, ambaye alipanda mwendokasi akitokea Ikulu, akiwa na ugeni wake, alisema mradi huo wa barabara ya juu utakuwa na ghorofa tatu.
"Magari kutoka njia zote nne yatapita hapa bila kusimama. Kwa hiyo madereva ambao watakuwa hawajui kuendesha kule juu, itabidi wawaajiri watu wawasaidie kuendesha kule juu," alisema.
Alisema barabara hiyo itakapokamilika, itatoa sura ya pekee kwa jiji la Dar es Salaam. "Kwa mfano, barabara ya Sam Nujoma kwenda Buguruni, itakuwa inapita juu, haya ni maendeleo ya pekee."
Rais Magufuli alisema mradi huo utagharimu sh. bilioni 188.71, kati ya fedha hizo, Benki ya Dunia itatoa sh. bilioni 186.725, kwa ajili ya usanifu, usimamizi na ujenzi wa mradi na serikali imetoa sh. bilioni 1.985, kwa ajili ya kushughulikia huduma nyingine.
"Huu sio mradi wa kwanza kufadhiliwa na Benki ya Dunia. Wamefadhili mingi, hivi sasa Benki ya Dunia imefadhili miradi 28, yenye thamani ya takribani Dola bilioni 4.2," alisema.
Kuhusu msongamano jijini Dar es Salaam, alisema suala la kuhamia Dodoma litapunguza pia msongamano wa magari kwa sababu watumishi hao watahamia huko na magari yao.
Pia, alisema sasa hivi wameanza kujenga kituo cha ICD, maeneo ya Ruvu, ambapo mizigo inayotoka bandarini, itakuwa inasafirishwa moja kwa moja mpaka Ruvu na magari yanayobeba mizigo hiyo yataichukulia hapo.
"Na kwa bahati nzuri, Benki ya Dunia tayari imeshakubali kutupa Dola milioni 300, ambazo zitasaidia kufanya matengenezo ya reli kutoka bandarini kwenda Ruvu na hii itapunguza msongamano kwa sababu magari makubwa hayataruhusiwa kuja jijini la Dar es Salaam," alisema.
Kuhusu barabara ya Dar es Salaam, Bagamoyo hadi Msata, alisema imeshakamilika, hivyo mabasi na malori hayatalazimika kupita Ubungo kwa sababu inatarajiwa kufunguliwa muda si mrefu.
Vilevile, alisema wanatarajia kujenga kilomita 120 za barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze.
"Tupo kwenye mchakato wa hatua za mwisho ili barabara hii ianze kujengwa," alisema Rais Dk. Magufuli.
RAIS BENKI YA DUNIA AMWAGA SIFA
Kwa upande wake, Rais wa Benki ya Dunia, Dk. Jim Yong Kim alisema: "Nimesikia sifa nzuri za Rais Magufuli kutoka nchi mbalimbali ndiyo maana nimekuja leo."
Alisema alipokuwa mdogo, alisoma maandiko ya Nyerere kwamba, maendeleo ni maendeleo ya watu, hivyo alivutiwa na kauli hiyo.
"Tuna imani na Tanzania na uwezo wake wa kufikia nchi ya uchumi wa kati," alisema Dk. Kim.
MAKONDA ASHUKURU
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema ujenzi huo utatatua kero ya msongamano wa magari, ambao umepoteza fedha nyingi za wananchi.
Aidha, alimshukuru kwa ujenzi wa barabara ya Mawasiliano, ambayo Aprili 11, mwaka huu, watafungua zabuni ili ianze kujengwa.
PROFESA MBARAWA ATOA AHADI
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema atahakikisha anausimamia mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.
Alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za ajira, ambazo zitapatikana kwenye ujenzi wa mradi huo.
"Nitawahimiza ili waweze kutoa ajira kwa Watanzania, waweze kujikwamua kiuchumi,"alisema Profesa Mbarawa.
MKURUGENZI TANROADS AFAFANUA
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Christianus Ako, alisema ujenzi wa barabara hizo zitakuwa za ngazi tatu.
Alisema usanifu wa barabara hiyo unalenga kupunguza uwezekano wa magari kukutana katika makutano kwa kunyanyua juu baadhi ya barabara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment