Monday, 20 March 2017

WADAIWA SUGU KODI YA ARDHI DODOMA WAONYWAOFISI ya Ardhi Kanda, imewataka wamiliki wa ardhi wenye madeni makubwa, kulipa malimbikizo ya kodi zao haraka, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari, mjini hapa, jana, Kaimu Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kati, Hezekiely Kitilya, alisema tayari wadaiwa hao wamepelekewa hati za madai, zikiwataka kulipa madeni yao ndani ya siku 14.

Kaimu Kamishna alisema, wizara inatoa wito kwa wadaiwa sugu wote kulipa malimbikizo yao ya madeni mara moja.

“Vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kufutiwa miliki zao na kuwapeleka mahakamani na hatimaye kukamata mali zao pamoja na kupiga mnada ili kufidia madeni yao,”alisema.

Alisema pamoja na changamoto zinazowakabili ya wananchi kutoona umuhimu wa kuwa na nyaraka za miliki, ofisi ya kanda hiyo imepiga hatua kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji kodi.

Kitilya alisema kanda ilipangiwa kukusanya sh. milioni 700, lakini hadi kufikia Februari, mwaka huu, ilikuwa imekusanya sh bilioni 1.04 za kodi ya ardhi.

Alisema mafanikio mengine ni kuratibu na kufuatilia utoaji wa hatimiliki za kimila 867.

“Utoaji wa hati za kimila unatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999. Mpaka Februari, mwaka huu, jumla ya hatimiliki za kimila 1,376, sawa na asilimia 159 ya lengo, tayari zimetolewa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali,”alisema.

Alisema hatimiliki hizo zimetolewa kwenye Halmashauri za Wilaya ya Manyoni, kwenye vijiji 13 na Halmashauri ya Mpwapwa kwenye vijiji 25 na Chamwino kijiji kimoja.
 

No comments:

Post a Comment