Monday 20 March 2017

UVCCM: KINGUNGE ANAFUNGA BANDA WAKATI FARASI KESHATOKA


UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM ), umemtaja na kumtaka mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, kunyamaza kimya kwa sababu ndiye muasisi wa uasi,na usaliti, na hata kuhamia kwake upinzani ni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa usaliti, ambao umekwama baada ya mgombea aliyemtaka, Edward Lowassa, kukosa sifa na vigezo.

Pia, umoja huo umeeleza kuwa, mzee huyo alifikiri CCM kitakuwa miliki yake na kwamba, angeweza kuamuru au kushurutisha jambo lolote lifuatwe kwa nguvu na ushawishi wake, bila kuheshimiwa kwa mipaka ya katiba na taratibu za uchaguzi.

Msimamo huo ulitolewa jana na Kaimu Katiba Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka,  kufuatia matamshi na shutuma zilizotolewa na Kingunge, akiwatuhumu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM,  Abdulrahman Kinana, akidai wameshiriki uasi na usaliti katika uteuzi wa mgombea urais mwaka 2015.

Shaka alisema wakati umefika kwa mzee huyo kukaa kimya na kurudi kijijini kwake Kipatimu huko Kilwa mkoani Lindi,  kulea wajuu na kutubia kwa Mungu asiyeamini kama yupo, kwa sababu alitaka kuichezea CCM, matokeo yake CCM ikamcheza na kumgaragaza hadi kufutika katika ramani ya kisiasa nchini.

Alisema kulingana na kumbukumbu za uasi na usaliti ndani ya CCM, mwanachama pekee anayeonyesha rekodi chafu ni Kingunge, ambaye aliwahi hata kutaka kuikwamisha Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere, wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Singida na mbunge, hadi akafukuzwa serikalini.

"UVCCM tunajua fika mzee Kingunge haamini uwepo wa Mungu, ndiyo maana anakuwa jasiri na mahiri wa kuongopa. Kama ni uasi na usaliti, yeye ndiye bingwa wa kuchongea wenzake kwa siasa za majungu. Alichochea kufukuzwa kwa Mzee Aboud  Jumbe, akishirikiana na kina Seif Shariff Hamad, hakuogopa aliisaliti hata Serikali ya Mwalimu Nyerere ikwame," alisema Shaka.

Akijibu hoja na madai kwamba, vigogo hao watatu walikiuka na kuvunja taratibu za vikao katika kumteua mgombea, Shaka alisema hakuna kongozi wa CCM aliyevuruga utaratibu, kilichofanyika ni kuhakikisha mgombea yeyote mtoa rushwa, fisadi na anayetumia fedha kusaka madaraka ya urais, hapiti na kuteuliwa.

"Chama chetu mapema kabisa kiliweka msimamo bayana, mgombea atakayebainika kutumia rushwa, anayegawa fedha na mwenye tuhuma za ufisadi au aliyekosa maadili ya uongozi, hateuliwi kuwa mgombea urais na kupeperusha bendera ya CCM. Kingunge na wenzake walifikiri mzaha mwisho wakajionea umadhubuti wa CCM," alieleza Shaka.

Alisema kama ni tabia ya usaliti, kupika  majungu, kuchongea viongozi wenzake kwa maslahi binafsi na kujipendekeza kwa viongozi wa juu, utamaduni huo uliasisiwa na Kingunge hadi akapachikwa jina bandia la "Mzee wa Fitna" .

"Mzee Kingunge alifikiri huku akidhani baada ya wazee kina Mwalimu Nyerere, Sheikh Thabit kombo, Mzee Rashid Kawawa kufariki, angejitwika dhamana ya uasisi na watu wamuogope kwa kila atatakalotaka. CCM ni taasisi, sio kampuni binafsi ya mtu na wapambe wake,"alisisitiza.

Shaka alimtaja Kingunge kwamba, bado ana machungu ya mtu aliyembeba mbelekoni na kumuahidi angekuwa mgombea urais kukwama, hatimaye wakajikuta wakihamia upinzani na kufikiri wangekuwa na ubavu wa kuing'oa CCM madarakani.

Alisema katika kusimamia masuala ya msingi ndani ya CCM, hakuna urafiki, kujuana, ujamaa au kubebana na kwamba, Lowassa na Kingunge walitaka kuleta mzaha wa kigezo cha Kikwete, Mangula na Kinana kujuana na Lowassa, akafikiri wangeweka katiba pembeni na masharti ya uchaguzi ili wavunje taratibu,"alieleza kongozi huyo wa UVCCM.

"Mzee Kingunge bado anaugulia jeraha na kidonda kibichi baada ya kukikwaa kisiki cha mpingo cha CCM. Yeye, Lowassa na washirika wao hawatasahau kile kilichotokea mwaka 2015.  CCM imekata jina la mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, vipi basi ishindikane kukata jina la Lowassa?"Alihoji Shaka.

Aidha, Shaka alimtaka Kingunge aache kutoa matamshi ya kutunga, badala yake akae kutafakari na hatimaye akubali kuamini imani yotote ya dini ili kumsujudia Mungu kwa sababu muda na umri wake kushiriki siasa umemtupa mkono na hadithi au madai anayoyatoa yanamsuta mwenyewe katika jamii .

Pia, Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM,  alieleza kuwa anaelewa kuwa matarajio ya Mzee Kingunge kisiasa wakati akihamia CHADEMA, alifikiri anajiunga katika  chama cha siasa, lakini alioyakuta huko ni tofauti na matarajio yake  na kujikuta akiikumbuka CCM aliyoisaliti na kufanya uasi.

"Mzee Kingunge nafikiri akipata usingizi, anaweweseka kwa kuwakumbuka Kikwete, Mangula na Kinana. Wenzake wamesimamia maslahi ya umma , wameongozwa na uzalendo kuliko urafiki na ushabiki wa kununuliwa, sifa na umadhubuti wa CCM huwezi kuukuta katika chama kingine,"alieleza Shaka.

Alisema iwapo Kingunge ataendelea kulalamika katika magazeti, hataweza kurudisha nyuma muda na wakati au kuanza tena upya  kwa mchakato wa kumpata mgombea wa urais wa mwaka 2015, kwa madai kuwa ng'we hiyo imeshapita na Ikulu yuko Rais aliyechaguliwa na Watanzania, Dk. John Magufuli.

No comments:

Post a Comment