Monday 20 March 2017

MAJALIWA AMWAKILISHA JPM UZINDUZI JUKWAA LA UCHUMI


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasili nchini Mauritius jana, kwa ajili ya kumuwakilisha Rais Dk. John Magufuli, katika mkutano wa kuzindua Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP).

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seewoosagur Ramgoolam, Waziri Mkuu Majaliwa alipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius, Vishnu Lutchmeenaraidoo.

Uzinduzi wa jukwaa hilo unatarajiwa kufanyika leo, mjini Port Louis, ambapo utawakutanisha viongozi wakuu wa nchi za Afrika, wanazuoni, wafanyabiashara na watu kutoka kwenye asasi mbalimbali za kiraia barani Afrika.

Pamoja na kuhudhuria mkutano huo, Waziri Mkuu, ambaye ameambatana na mkewe, mama Mary Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Mauritius, litakalofanyika Machi 23, 2017.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa baada ya kumaliza mkutano huo, anatarajia kutembelea maeneo maalumu ya uwekezaji, viwanda vya sukari na nguo.

Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na maofisa wengine wa serikali.

No comments:

Post a Comment