Monday 20 March 2017

52 WAJITOSA KUWANIA UBUNGE WA EAC KUPITIA CCM


IDADI kubwa ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), imejitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), zilizoanza kutolewa jana.

Fomu hizo zilianza kutolewa saa tatu asubuhi, katika Ofisi Ndogo za CCM zilizoko mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, ambapo hadi saa saba mchana, waliojitokeza walikuwa 26.

Baadhi ya walijitokeza kuchukua fomu hizo ni aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu Kawawa, Bakili Mwanukuzi na aliyewahi kujitokeza kuchukua fomu ya urais na uspika, Leonce Mulenda.

Wakizungumza baada ya kuchukua fomu, Mulenda alisema ameamua kugombea ili kutatua kero mbalimbali zilizopo Afrika Mashariki, ikiwemo suala la mafuta na madini.

Alisema anaamini kuwa CCM ndiyo chama pekee nchini kitakachoweza kuwakomboa Watanzania kuelekea maisha bora.

"Unajua wapo watu wanaodhani kuwa kipo Chama kinachoweza kuwa mbadala wa CCM, katika kuwaletea maendeleo wananchi. Fikra hizo ni potofu kabisa, CCM bado ndicho chama pekee imara na chenye sera bora zinazotekelezeka, tofauti na vyama vingine," alisema Mulenda, ambaye ana kadi ya CCM yenye namba Ab 1353192.

Mulenda alisema anaamini CCM ndicho chama kinachofaa kuongoza Watanzania kwa sababu ya uwezo wake, ambao umejengwa chini ya misingi imara, iliyowekwa na muasisi wake, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, tangu enzi za Tanganyika African National Union (TANU), ambacho CCM inaendeleza misingi yake.

Aidha, alisema kilichowafanya baadhi ya watu kudhani CCM sio chama cha wanyonge, ni kutokana na baadhi ya viongozi kusahau au kuipuuza misingi hiyo iliyowekwa na Baba wa Taifa, hivyo kuanza kujiwekea misingi bandia kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi.

"Baada ya Tanzania kumpata Rais Dk. John Magufuli, hali inaelekea kubadilika na huenda ikaimarika kabisa kutokana na Rais anavyojaribu kuiweka nchi katika misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Hayati Karume," alisema Mulenda.

Kwa upande wake, Zainabu alisema ameamua kugombea kwa sababu ana uzoefu wa kutosha, ambao ameupata kutoka ndani ya Chama.

Alisema Chama kimemlea na kutokana na umri wake kuwa mdogo, ameona ipo ya haja ya kugombea ili kuwasaidia Watanzania.

"Endapo nikichaguliwa, nataka kuwa mbunge wa Watanzania wote, nataka niwaonyeshe vijana fursa zilizopo ndani ya EAC, maana kuna baadhi hawazijui fursa hizi," alisema.

No comments:

Post a Comment